NYASA, NAMTUMBO WATENDAJI WAWEKWA KWENYE UTAYARI KUKABILIANA NA EL NIÑO, EBOLA
Posted on: September 30th, 2026Na Atley Kuni, WAF-Ruvuma
Watendaji wa Wilaya za Nyasa na Namtumbo mkoani Ruvuma wameendelea kuwekwa tayari kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño pamoja na tishio la ugonjwa wa Ebola, huku jamii ikitakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuchukua tahadhari na kutoa taarifa mapema.
Akiongea Septemba 30, 2026 kwenye kikao kilicho wakutanisha watendaji hao mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Chipole Mpelembe amewataka kuimarisha mifumo ya tahadhari na mwitikio wa haraka, kutambua maeneo hatarishi, kuhakikisha miundombinu ya maji inakuwa salama na kujiandaa na vifaa muhimu vya dharura ili kupunguza madhara yanayoweza kuwapata wananchi.
Akiongea wilayani Namtumbo Chipole amewataka watendaji hao kutekeleza mpango wa kisekta unaohusisha afya, maji, miundombinu, kilimo na mifugo, ikiwemo kusafisha mifereji na makaravati, kulinda vyanzo vya maji, kuandaa vifaa vya uokoaji na kutambua maeneo salama kwa waathirika endapo majanga yatatokea.
Kwa upande wa Ebola, Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha timu za mwitikio wa haraka pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya nchini huku wananchi wakihimizwa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka kugusa majimaji ya mwili ya mtu mwenye dalili pamoja na kutoa taarifa mapema wanapoona viashiria vya ugonjwa huo.
Wizara ya Afya pia imesisitiza kuwa utayari wa kukabiliana na majanga hauwezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi. Jamii inapaswa kufuatilia taarifa rasmi, kuzingatia maelekezo ya wataalamu, kushiriki katika usafi wa mazingira, kuzibua mitaro na kuhakikisha maeneo ya makazi hayawi hatarishi wakati wa mvua kubwa.
Katika hatua hiyo, wananchi wa Nyasa na Namtumbo wametakiwa kuchukulia tahadhari hizi kama jukumu la pamoja, kwa kuwa maandalizi ya mapema, utoaji wa taarifa kwa wakati na ushirikiano kati ya jamii na mamlaka vinaweza kusaidia kupunguza madhara na kulinda afya, maisha na mali za wananchi.