Wizara Ya Afya

DKT. SAMIZI: M-MAMA MFANO WA MAFANIKIO YA AFYA KIDIJITALI

Posted on: September 30th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Kigali, Rwanda

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence George Samizi, amesema mfumo wa m-mama ni miongoni mwa mifumo ya afya kidijitali iliyothibitisha mafanikio nchini Tanzania na unaoonesha namna teknolojia inaweza kutumika kuboresha huduma za dharura kwa mama wajawazito na watoto wachanga.

Dkt. Samizi ameyasema hayo Septemba 30, 2026 jijini Kigali, Rwanda, wakati akimwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika Mkutano wa Afrika wa Teknolojia za Afya 2026, kwenye mjadala wa pamoja uliohusu namna ya kufanya mifumo iliyothibitisha mafanikio iweze kufadhiliwa na kupanuliwa kwa kiwango kikubwa.

Amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021, mfumo wa m-mama umewezesha kuratibu zaidi ya rufaa za dharura 214,000 za mama wajawazito na watoto wachanga, hatua inayosaidia kuhakikisha wanaohitaji huduma za dharura wanapata usafiri na kufikishwa katika vituo vya afya kwa wakati.

Amesema kupitia mfumo huo, matumizi ya magari ya wagonjwa katika huduma za dharura yameongezeka kutoka takribani asilimia 60 hadi zaidi ya asilimia 80, jambo linaloonesha mchango wa teknolojia katika kuimarisha uratibu wa huduma za usafiri wa wagonjwa.

Dkt. Samizi amesema mafanikio ya m-mama yanaonesha umuhimu wa kuwekeza katika mifumo ya kidijitali inayozingatia changamoto halisi za wananchi, huku taarifa zinazopatikana kupitia mfumo huo zikisaidia Serikali kufuatilia huduma, kutambua changamoto na kufanya maboresho kwa wakati.

Amesema Tanzania sasa inalenga kuhakikisha mifumo iliyothibitisha mafanikio kama m-mama haibaki katika maeneo machache pekee, bali inaendelea kupanuliwa na kuunganishwa na mifumo mingine ya afya ili kuongeza ufanisi na kufikia wananchi wengi zaidi.