Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAKUTANA NA WADAU WA SEKTA YA AFYA, YAWAPITISHA KWENYE SHERIA YA MFUKO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE.

Posted on: December 14th, 2023

Na WAF Dar Es Salaam.

Wizara ya Afya kupitia Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe pamoja na wataalam wamekutana na Wadau wa Maendeleo wa Sekta ya Afya nchini na kujadili namna wanavyoweza kushirikiana katika utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao hivi karibuni imesainiwa hivi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi hicho, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amesema wadau hao ni muhimu katika sekta hivyo wanaguswa moja kwa moja katika utekelezaji wa Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote na muhimu kukutana kwa pamoja na kuweza kuipitia Sheria hiyo, itakayowaongoza katika utekelezaji.

Kwa upande wake mwakilishi wa Wadau wa Maendeleo katika Sekta ya afya, ambaye pia ni Mwakilishi kutoka Ubalozi wa Uingereza Bi.Gertude Mapunda, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu kwa kuweza kusaini na kukubali Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote kuanza kutumika nchini na kuahidi kuwa Wadau wa maendeloe wapo tayari kushirikiana na Serikali katika kufikia azma ya Bima ya Afya kwa wote.

“Kuja kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote itakuwa ni msaada mkubwa kwa Watanzania walio wengi, kwani kutokana na unafuu wake utasaidia wengi kujiunga na kuwa wanachama na kufanikisha upatikanaji wa huduma za afya kuwafikia walio wengi” Amesema Bi Getrude.

Katika kikao hicho Wadau wa Maendeleo katika Sekta ya Afya wamefanikiwa kupitishwa kwenye Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote, namna mfuko huo utakavyotekelezwa na pia wamepata wasaa wa kujadiliana masuala mbalimbali yatakayojitokeza pindi mfuko huo utakapoanza kutekelezwa.