Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAKAMILISHA MAJENGO YA HUDUMA ZA DHARURA

Posted on: May 14th, 2023

-lengo ni kupunguza asilimia 40 ya vifo

Na WAF - Dodoma

Serikali imefanya mapinduzi makubwa katika Sekta ya afya kwa kuweka mfumo madhubuti wa huduma za dharura na ajali kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya ambapo matokeo ya uwekezaji huo ni kupunguza vifo kwa 40% ndani ya hospitali na kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma hizo nchini.

Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2023/2024 kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alisema kuwa mapinduzi hayo ni makubwa kufanyika katika Sekta ya Afya tangu Tanzania ipate Uhuru.

Waziri Ummy alisema, Wizara imeendelea kukamilisha ujenzi wa majengo 23 ya kutoa huduma za dharura (EMD) katika Hospitali Maalum, Kanda na Mikoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba.

Aidha, Serikali ya awamu ya sita kupitia OR-TAMISEMI imewezesha ujenzi wa majengo ya EMD 80 katika ngazi ya Hospitali za Halmashauri. Jumla ya majengo ya kutoa huduma za dharura (EMD) yamefikia 118 kutoka 8 mwaka 2021. "Haya ni mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya hapa Tanzania tangu uhuru kwa Serikali kuweka mfumo madhubuti wa huduma za dharura kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya, matokeo ya uwezekaji huu yatapunguza vifo ndani ya Hospitali kwa asilimia 40 na kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma za dharura." Alisema.

Kwa upande wa huduma za matibabu ya Kibingwa na ubingwa Bobezi Waziri Ummy alisema kuwa, Wizara imeendelea kuboresha na kuimarisha huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi nchini kwa kusogeza huduma hizi karibu na wananchi kwa kuendesha kambi mbalimbali za matibabu ya mkoba ikiwa pamoja na huduma za ushauri, upasuaji na matatizo mbalimbali.

Alisema, katika kipindi cha Julai 2022 hadi machi 2023 jumla ya wagonjwa 80,018 walihudumiwa kupitia mpango huo “mpango huo umewezesha wananchi kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa gharama nafuu, Serikali itaendelea kuimarisha huduma hizi ili ziweze kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kugharamia huduma husika.” alisisitiza.