WIZARA YA AFYA YAJIRIDHISHA NA VIWANGO VYA UTOAJI WA HUDUMA HOSPITALI YA MKOA SINGIDA
Posted on: February 10th, 2025
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Huduma za Kinywa na Meno Wizara ya Afya Dkt. Baraka Nzobo ameridishwa na uboreshaji wa huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.
Kiongozi huyo kutoka Wizara ya Afya mapema Februari 7, 2025 aliambatana pia na jopo la wataalam kutoka Wizara hiyo yuko mkoani Singida kwa lengo la kuendesha zoezi la usimamizi shirikishi katika hospitali hiyo na baadhi ya maeneno ya Mkoani Singida.
Jopo la Wataalam wa Wizara ya Afya kutoka Idara ya Tiba wamefikia hatua hiyo, mara baada ya kujionea hali ya utoaji wa huduma za Afya kwa wananchi inavyoendelea sambamba na usafi, ubora wa huduma zote zinavyotolewa kwa kufuata miongozo yote ya sekta ya Afya.
Awali Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida Dkt. David Mwasota ameishukuru Serikali na Wizara kwa kuendelea kuwapa ushirikiano wa hali ya juu ambao umelenga zaidi kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Singida na Watanzania kwa ujumla.
Dkt. Mwasota ameongeza kwa kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuwekeza katika hospitali hiyo hususani katika huduma za wagonjwa mahututi.
“Kwa sasa kuna jengo maalum kwa wagonjwa mahututi (ICU) linalotoa huduma kwa kiwango cha juu, vilevile mashine mbalimbali kama CT Scan, Digital X ray machine kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa Singida na kupunguza rufaa kwa kiasi kikubwa,”. Alisesema Dkt. Mwasota.