Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAENDELEA KUIMARISHA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA ( STAR RATING ASSESEMENT) SIMIYU

Posted on: October 26th, 2026

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI kwa kutumia timu ya Wataalam Kitaifa inaendelea kufanya tathmini ya Vituo vya kutolea huduma za afya ya Msingi (Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali katika ngazi ya Halmashauri zote za mkoa wa Simiyu kwa kuvipatia kategoria ya nyota kulingana na huduma zinayotolewa kwa lengo la kuinua na kuimarisha ubora wa huduma za afya zinazotolewa kwa Wananchi.

Akizungumza leo oktoba 26 ,2026 mkoani Simiyu wakati wa kuanza kwa tathmini hiyo Dkt. Radenta Bahegwa Afisa Uimarishaji Ubora, Kitengo cha Uhakiki ubora huduma za afya Wizara ya Afya, amesema tathmini hiyo imeanza leo katika Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu na itaendelea kwa muda wa wiki mbili.

Dkt.Radenta amesema lengo la kufanyika kwa tathmini hiyo ni juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya katika Vituo vyote vya kutolea huduma za afya hapa nchini.

"Zoezi la star rating assessment of all primary Healthcare facilities" ni maalum kabisa kwa ajili ya kuangalia Ubora wa huduma za afya katika Vituo vyote na kuvipa kategoria ya nyota kuanzia 0 hadi 5 kulingana na Ubora wa huduma katika Kituo husika" amesema Dkt. Radenta.

Aidha,amesisitiza kuwa mpango huu wa uboreshaji wa huduma za afya katika Vituo vya kutolea huduma unaenda sambamba na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote awamu ya pili uliozinduliwa rasmi Oktoba 22, 2026 na Waziri wa Afya Mhe.Mohamed Mchengerwa.

Amesisitiza kuwa nia na malengo ya Wizara ya Afya ni kuhakikisha Wananchi wanaendelea kupata huduma za Afya zenye uhakika na ubora karibu na maeneo wanayoishi.

Katika kufikia malengo ya utoaji wa huduma bora za Afya kwa Watanzania kupitia Bima ya Afya kwa wote Serikali kupitia Wizara ya Afya imeweka malengo ya kuhakikisha vituo vyote vinafikia angalau kiwango cha nyota 3 hadi 5 ambavyo ni viwango vinavyokidhi ubora wa huduma kulingana na viwango vya Kitaifa kuelekea ithibati za Kimataifa (Accreditation).