Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA, BENKI YA DUNIA ZAJADILI KUFANIKISHA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: November 22nd, 2024

Na WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Novemba 21, 2024 amekutana na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayewakilisha Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe Bw. Nathan Belete aliyeambatana na Msimamizi wa Miradi ya Afya wa Benki ya Dunia Kanda Namba Moja ya Afrika Bw. Ernest Massiah kwa lengo la kujadiliana namna ya kufanikisha Bima ya Afya kwa Wote.

Mkutano huo umefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Mhagama amesema ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia umewezesha kupatikana maendeleo makubwa ya utekelezaji wa mpango ya uwekezaji wa afya ya mama na mtoto nchini (TMCHIP) ikiwemo kupunguza vifo pamoja na msaada wa kifedha na kiufundi unaotolewa na Benki ya Dunia.

Waziri Mhagama amesema ni muhimu kuanzisha mfuko wa wadau wa maendeleo (Multi-Donor Trust Fund) ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa endelevu na kuratibu misaada ya wafadhili katika kutekeleza ajenda za afya za muda mrefu kama Bima ya Afya kwa Wote, mpango jumuishi wa watumishi ngazi ya jamii (CHWs).

“Vilevile utaimarisha mifumo ya utayari wa kukabiliana na dharura, maafa, magonjwa ya mlipuko, magonjwa yasiyoambukiza na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, tukikamilisha haya ushirikiano huu utakuwa mzuri zaidi kwakuwa hivi vyote ni vipaumbele vya Rais Dkt. Samia," amesema Waziri Mhagama

Aidha, Waziri Mhagama ametoa shukrani kwa msaada wa Benki ya Dunia kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia ambapo amewahakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano zaidi ili kutekeleza malengo ya Sekta ya Afya kwa manufaa ya watanzania wote.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Bw. Nathan Belete ameelezea furaha yake kwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Tanzania pamoja na Benki ya Dunia ambapo maendeleo makubwa yamepatikana kupitia mpango wa uwekezaji wa afya ya mama na mtoto (TMCHIP) vilevile wameahidi kutoa dola za kimarekani Milioni 500 kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa miradi ya afya (UHI)," amesema Bw. Belete