Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WHO YATANGAZA MPOX DHARURA YA KIAFYA KIMATAIFA

Posted on: August 15th, 2024



Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko wa ugonjwa wa mpox (homa ya nyani) katika baadhi ya nchi za Afrika kuwa dharura ya afya ya umma ambayo inaleta hofu kimataifa.


Ugonjwa huo unaoambukiza kwa haraka umeshaua takribani

watu 450 tangu ulipuke katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.


Ugonjwa sasa unatajwa kuenea katika maeneo ya Afrika ya kati na mashariki, huku wanasayansi wakiwa na wasiwasi kuhusu jinsi aina mpya ya ugonjwa huo inavyoenea na kiwango chake cha juu cha vifo.


Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema uwezekano wa kuenea zaidi kwa ugonjwa huo ndani ya Afrika na kwingineko "ni jambo linalotia wasiwasi sana."


"Ushirikiano na uratibu wa kimataifa ni muhimu ili kukomesha kusambaa kwa janga hili na kuokoa maisha ya watu," amesema.


Mpox huambukizwa kupitia ukaribu wa mgonjwa kwa asiye mgoniwa kama vile kufanya ngono, kugusana ngozi na kuzungumza kwa karibu ama kupumuliana hewa.


Husababisha dalili kama za homa, mafua, malengelenge hadi vidonda vya ngozi na inaweza kusababisha kifo. 


Takwimu zinaonesha watu wanne kati ya 100 wanaokumbwa na ugonjwa huo hufariki dunia.


Mlipuko wa ugonjwa mpox umeelezwa kwamba unaweza kudhibitiwa kupitia chanjo, ingawa kwa sasa chanjo hupatikana kwa watu walio hatarini au wale ambao wamewasiliana kwa karibu na mtu au watu walioambukizwa.