WEKENI MIKAKATI YA PAMOJA KATIKA TIBA ASILI TUIDUMISHE
Posted on: January 31st, 2025
Na WAF – DAR ES SALAAM
Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Afya zimetakiwa kuweka mikakati madhubuti ya ushirikiano katika sekta ya tiba asili ili huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya usalama na ufanisi.
Hayo yamesemwa Tarehe Januari 31,2025 na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, Dkt. Hemed Nyembea wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kujadili Mikakati ya Afya na Huduma za Tiba Asili, Mkoani Dar es salaam
“ Tiba za asili imekuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya watu kwa karne nyingi na katika miaka ya hivi karibuni, tumepiga hatua kubwa, ikiwa ni pamoja na kuingiza huduma za tiba asili zipatazo saba katika hospitali saba za rufaa nchini. “ Amesema Dkt. Nyembea
Dkt. Nyembea amesema Ushirikiano huu unapaswa kuhusisha taasisi za utafiti, vyuo vya elimu ya juu, na wadau wa tiba asili ili kuwezesha tafiti za kina, usajili wa dawa, na uboreshaji wa mifumo ya udhibiti.
Ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wote, hususan taasisi za utafiti na elimu ya juu kwa mchango wenu wa hali na mali katika kuhakikisha sekta ya tiba za asili inakua na kustawi kwani Ushirikiano wenu ni muhimu sana kwenye kufanikisha malengo yetu ya muda mrefu.” Ameongeza Dkt. Nyembea
Aidha, Dkt. Nyembea ameitaka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya tafiti za kina kwa wataalamu wa tiba asili ya Mwafrika kwani NIMR inapaswa kufanya tafiti za kina kuhusu vyanzo vya dawa zinazotumika na kuhakikisha kuwa zinatunzwa vizuri na kuendelea kuzalishwa kwa wingi kwenye huduma zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, Prof. Joseph Otieno, ameeleza kuwa dawa zinazotengenezwa na wataalamu wa tiba asili zimepiga hatua kubwa katika ubora, usalama, na ufanisi.
Ushirikiano wetu utaendelea kuwa chachu ya mafanikio katika kukuza tiba asili kwa manufaa ya taifa letu kwa kizazi cha sass na kijacho.