WEKENI MAZINGIRA RAFIKI KWA WAZALISHAJI WA DAWA ZA TIBA ASILI, TIBA MBADALA
Posted on: May 27th, 2024
Na WAF - DAR ES SALAAM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ameitaka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuhakikisha inaweka mazingira yatakayo wajengea uwezo wazalishaji wa Dawa za Tiba Asili/Mbadala kuimarika na kukua ili Dawa zao zisaidie kuponya jamii.
Dkt. Jingu amesema hayo leo Mei 27, 2024 wakati alipotembelea Ofisi za Mkemia Mkuu wa Serikali, Jijini Dar Es Salaam ambapo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya ofisi hiyo na wazalishaji wa Dawa za Tiba Asili/Mbadala
Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha eneo la Tiba Asili/Mbadala linakuwa miongoni mwa maeneo ambayo yanapewa kipaumbele ili kusaidia jamii katika kuponya kama ilivyokuwa wakati wa Corona.
"Tuwasaidie Wataalamu wetu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala, sisi kama Wizara tuna nafasi yetu na nyie (Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali) Mnanafasi yenu ya kuja na Maoni,Mawazo au njia zitakazosaidia tutatekelza hili sababu pia juzi kwenye vipaumbele vya Wizara Bungeni ni moja ya eneo ambalo tumelibainisha kama tutaweka mkazo mkubwa na wote mnajua wakati wa COVID zilitusaidia sana" amesema Dkt. Jingu
Dkt.Jingu pia amesisitiza Ofisi ya Mkemia Mkuu wa serikali isaidie kuwajengea uwezo watoa Huduma, wazalishaji na wamiliki wa viwanda vya dawa za Tiba asili na Tiba Mbadala ili wafanye bunifu zao Vizuri ili bidhaa zao watazo zalisha ziweze kuisaidia jamii yetu.
Kufuatia Ripoti iliyosomwa na Meneja Maabara ya Sayansi Jinai Bailojia na Vinasaba Fidelis Bugoye kuainisha uwepo wa changamoto ya Baadhi ya jamii kukwamisha Mchakato wa kupata za ushidi wa vinasaba hasa katika Maswala ya haki jinai, Dkt.Jingu ametoa rai kwa jamii kutoa ushirikiano kwa Mamlaka za Uchunguzi hasa Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuimarisha utatuzi wa Masuala ya haki jinani nchini.
"Mkemia Mkuu wa Serikali anajukumu kubwa katika kuimarisha mnyororo Mzima wa haki jina katika nchi yetu, changamoto inayowakabili ni ushirikiano kutoka kwa wanajamiii, kwahiyo nitoe wito kwa wanajamii kutoa ushrikiano kwa Ofisi ya Mkemia ili kuimarisha utendaji kazi wake" amesema Dkt. Jingu.