Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI UMMY MWALIMU AWATOA HOFU WATANZANIA KUHUSU EBOLA

Posted on: October 4th, 2022

Na. Catherine Sungura, WAF - KAGERA.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewatoa hofu Watanzania kuhusu Ugonjwa wa Ebola uliopo nchi jirani na kuwataka waendelee kuchukua tahadhari za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo wakati wa ziara ya kukagua utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo katika Mkoa wa Kagera wakati akipokea taarifa ya Mkoa huo kukabiliana na mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kagera akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Albert Chalamila.

"Tunatakiwa kuongeza jitihada za kuzuia ugonjwa huo usiingie hapa nchini,niwakumbushe wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote tunazoelekezwa na wataalamu wa afya kama vile kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni,kutokugusana mikono na uonapo dalili nenda kituo cha kutolea huduma za afya".

Hata hivyo Waziri Ummy alisema Wizara ya Afya itaendelea kutoa elimu kwa umma kwa Watendaji wote wa Vijiji, Kata na Tarafa pamoja na kutoa mafunzo kwa Waganga wa Tiba Asili ili kutambua mtu mwenye dalili za magonjwa ya mlipuko.

Aidha,Waziri Ummy amesema Waganga Wafawidhi 351 wa Vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Kageran watapewa mafunzo ya kukabiliana na Mlipuko dhidi ya Ugonjwa wa Ebola.

“Tutaupa kipaumbele Mkoa wa Kagera katika kukabiliana na tishio hili kwani mkoa huu eneo kubwa linapakana na nchi nyingi” amesema Waziri Ummy na kuahidi kufanya mazoezi ya utayari ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko (Simulation Exercises).

Kwa upande mwingine Waziri Ummy amewaahidi kuwapatia magari matati (3) ya kubebea wagonjwa (Ambulance) ili kuokoa maisha kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka mkoa hapo.

Naye, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Albert Chalamila amemuomba Waziri Ummy kujengewa kituo maalumu cha kutenga wahisiwa wa magonjwa ya mlipuko (Isolation Center)katika mpaka wa Mulongo pamoja na Wilaya ya Ngara-mpaka wa Rusumo, Murusagamba na Kabanga.

Hata hivyo Mhe. Chalamila ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuipatia hospitali ya Rufaa ya Mkoa CT-Scan pamoja na vifaa tiba vingine ambapo vimeanza kusimikwa hospitalini hapo.