Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI UMMY AWATAKA WATAALAMU KUJADILI KUONGEZWA KWA HUDUMA ZA AFYA YA AKILI KATIKA MFUKO WA BIMA YA AFYA.

Posted on: October 10th, 2022

Na WAF - DSM

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Wataalamu wa afya kujadili uwezekano wa huduma za afya ya akili kuwa sehemu ya huduma zinazogharamiwa na mfumo wa taifa wa Bima ya afya ili kupunguzia mwananchi gharama za matibabu.

Waziri Ummy ameeleza hayo leo Oktoba 10, 2022 katika Kongamano la kwanza la kitaifa la afya ya akili lililofanyika katika kituo cha kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

“Suala jingine ambalo nataka kulijadili, ni kwanini Bima ya Afya isikubali kugharamia huduma za Saikolojia na huduma nyingine za Afya ya Akili zisiwepo kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya” amehoji Waziri Ummy Mwalimu.

Sambamba na hilo aliendelea kwa kuwataka Wataalamu katika Kongamano hilo kujadili namna bora ya kuboresha huduma na kutoa maoni ya nini kifanyike ili kukabiliana na changamoto za Afya ya Akili na kuboresha Huduma za Saikolojia na Afya ya akili ili kuwezesha wananchi kupata huduma bora.

Aidha, Waziri Ummy amesema bado kuna changamoto ya ajira kwa vijana na kuwataka wadau kushirikiana na Serikali kuanzisha vituo vya utengamao wa afya ili wananchi waweze kupata huduma za Saikolojia na Afya ya Akili karibu zaidi katika maeneo yao walipo.

Amesema, nchini Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa takriban milioni 7 wenye magonjwa mbalimbali ya akili na matumizi ya dawa za kulevya, huku akieleza kuwa, miongoni mwao zaidi ya watu milioni1.5 wanaishi na ugonjwa wa Sonona (Depression).

Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema kufanyika kwa kongamano hili kutasaidia kupata michango tofauti kutoka kwa wadau muhimu wa afya ya akili juu ya fursa na changamoto zilizopo na kutoa mapendekezo ya kufikia suluhu ya utatuzi wa changamoto hizo.

Pamoja na hayo, Prof. Makubi amewashukuru na kuwapongeza timu yote ya maandalizi kwa kazi nzuri bila kusahau chama cha madaktari bingwa wa Afya ya Akili, Chama cha Wanasaikolojia na vyama vingine vya kitaaluma.