WAZIRI UMMY ALITAKA BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA YA AFYA KUIMARISHA UBORA WA HUDUMA
Posted on: April 4th, 2024
Na WAF, DODOMA
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, ameliambia Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya kugeukia na kuboresha kipengele cha ubora wa huduma kwa wananchi ili azma ya Serikali ya kufikisha huduma bora kwa wananchi mahala walipo iweze kufanikiwa.
Waziri Ummy ametoa wito huo Aprili 04, 2024 wakati wa kikao cha baraza hilo lililokutana kwa siku moja jijini Dodoma kwa ajili ya kupitia ya utekelezaji na ufafanuzi wa hoja mbalimbali pamoja na mikakati ya kutoa huduma bora kwa wananchi sambamba na kujadili bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 na 2024/25.
Waziri Ummy amelitaka baraza hilo, kuhakikisha linakuwa chombo sahihi cha kumshauri yeye na menejimenti ya Wizara ili changamoto zinazoikabili sekta ya afya ziweze kusuluhishwa kwa pamoja.
“Tunajua tumefanya vizuri sana kwenye miundombinu na vifaa tiba, lakini tumeendelea kulalamikiwa kwenye eneo la huduma na hususan ngazi ya msingi, huku juu kwenye kanda na ngazi ya hospitali za Rufaa za mikoa, tumejitahidi sana. Rai yangu kwenu tuendelee kusaidia katika kuimarisha huduma kwenye Zahanati, Hospitali za Wilaya na Vituo vya afya”. Amesema Waziri Ummy.
“Jambo tukishakubaliana kwenye vikao halali, tunatakiwa kwenda kwenye utekelezaji, tunapoendelea kuzunguka na kupiga dana dana tunawakwamisha wananchi na mwisho wa siku tunalaumiwa. Niliombe baraza hili, mnapojadiliana suala hili mlipe kipaumbele”. Amesema Waziri Ummy.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy ametumia Baraza hilo kuhimiza matumizi ya TEHAMA kwenye Sekta ya Afya, kwani ndio suluhu itakayo wezesha kuepusha udanganyifu, ikiwa pamoja na vipimo kurudiwa rudiwa, lakini pia matumizi mabaya ya vifaa tiba kama CT Scan.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu wakati akimkaribisha Waziri Ummy amemueleza kuwa kikao hicho kitajadili mada mbalimbali zikiwemo uwasilishaji wa bajeti, taarifa ya utekelezaji wa hoja mbalimbali za watumishi, rasimu ya miundo ya utumishi wa kada ya afya, utendaji kazi katika utumishi wa umma, Mkakati wa utoaji wa huduma na utendaji kazi wa wizara katika kuboresha huduma za Afya.