WAZIRI MCHENGERWA AZITAKA TAASISI ZA AFYA KUJITATHMINI KUELEKEA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Posted on: January 15th, 2026Na WAF, Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amezitaka Taasisi ambazo ziko chini ya Wizara ya Afya na Vituo vyote vya kutolea huduma kujitathmini utendaji kazi wake, mapungufu na changamoto na kuona namna gani ya kutatua changamoto hizo wakati Serikali ikielekea kwenye utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Waziri Mchengerwa amesema hayo Januari 14, 2026 jijini Dodoma katika kikao kazi kilichohusisha Wakurugenzi Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa na Watumishi wote wa Sekta ya Afya.
Mhe. Mchengerwa amesema Bima ya Afya kwa Wote italeta ongezeko la matumizi ya huduma za afya hivyo amevitaka vituo vyote vya kutolea huduma za Afya kuanzia ngazi ya msingi mpaka Taifa kuimarisha huduma wanazo zitoa.
“Wananchi waliokuwa wanajizuia kufika Hospitalini kwa sababu ya gharama sasa watafika. Huduma zitahitajika kwa wingi zaidi, kwa kasi zaidi, na kwa ubora unaofanana”, amesema Waziri Mchengerwa.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote bila uwepo wa huduma bora ni hatari kwa wananchi na Serikali, hivyo amesisitiza kuboresha viwango vya huduma, miongozo ya kitaaluma pamoja na kuwa na vibali vinavyokubalika kimataifa.
Ameongeza kuwa ubora wa huduma haupimwi kwa huduma zinazotolewa Maabara pekee bali ni nidhamu ya watumishi kuanzia mapokezi hadi mgonjwa anapotoka huku akisisitiza kuwa ubora wa sio neno la ripoti bali ni kitu kinachoonekana kwenye matokeo ya wagonjwa.
“Kila mmoja wetu ana nafasi, wajibu na mchango wa moja kwa moja wa ubora ili kuhakikisha Bima ya Afya kwa Wote inaanza kwa uthabiti, inasimamiwa kwa nidhamu na inalinda hadhi ya haki ya afya ya Mtanzania”, amesisitiza Mchengerwa.
Waziri Mchengerwa amesema Bima ya Afya kwa Wote siyo mradi wa muda mfupi unaotekelezwa ili kukamilisha ahadi ya kisiasa, wala si tukio la kuzinduliwa kwa shangwe kisha kuachwa lijiendeshe lenyewe. Ni mfumo wa kizazi, unaogusa maisha ya watu leo, kesho, na kwa miongo ijayo ambapo kila Mtanzania anatarajiwa kupata huduma bora za afya bila kujali uwezo wake wa kifedha.