Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAZIRI DKT. GWAJIMA AFIKA KITUO CHA MABASI MAGUFULI KUJIONEA TAHADHARI YA UVIKO 19

Posted on: December 21st, 2021

Na Atley Kuni, WAMJW, ARUSHA.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto,  Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezindua Kampeni Harakishi na Shirikishi kwa Jamii awamu ya pili na kusema, changamoto za uwepo wa UVIKO 19 ni changamoto kwa maendeleo ya dunia nzima ikiwemo na Tanzania. 

Dkt. Gwajima, ameyasema hayo leo Desemba 22, 2021, mkoani Arusha, ambapo Hafla hiyo imefanyika na kuhudhuriwa na Viongozi wa Serikali,  Dini pamoja na Jamii sambamba na Wananchi wa Arusha na Mikoa ya Jirani.

Akizindua Mpango huo, Dkt. Gwajima, amesema, katika kipindi cha kuanzia Mwezi Disemba, 2021 nchi yetu pia imeshuhudia kuendelea kuongezeka kwa maambukizi mapya ya UVIKO-19 kutoka maambukizi 14 kwa siku hadi 47 miongoni mwa wasafiri kwa takwimu za vipimo vya maabara kuu ya taifa. 

 "Mafanikio ya mapambano haya yanategemea zaidi jinsi gani Wakuu wa Mikoa na vyombo vyenu mmeendelea kujipanga kila siku, kwa kuboresha mikakati ya kuwafikia wananchi hadi ngazi ya mitaa, vijiji na vitongoji ili waelimike wajikinge na wapate huduma ya chanjo. Alisema Dkt. Gwajima.

Kampeni ya kaya kwa kaya ya kuwashirikisha viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji inadhamira ya kuona mikoa mingine inafanya na kupata mafanikio makubwa zaidi kama Mwanza, Kagera na Ruvuma ilivyofanikiwa.

Dkt. Gwajima ametumia fursa hiyo, kuwaomba, Viongozi wa Mikoa na Halmashauri wanakua bega kwa bega ili kufikia azma yakuchanja watu wapatao 4000 hadi 5000 kwa Mkoa na watu 80,000 hadi 100,000 kwa nchi nzima kila siku.

Akitoa taarifa wakati wa hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi alisema,  kwa sasa wameanza kufanya utafiti wa chanjo na wataendelea kutoa taarifa wapi tumefikia kwenye Chanjo hiyo,  aidha "kwa sasa nchi ina mitambo ya kufua hewa ya Oksijeni kwenye hospitali zetu, hii itasaidia kuokoa maisha kwa wahitaji wa hewa kama watoto njiti na wagonjwa wengine mahututi"  Prof.Makubi.

Akiongea kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa, Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa, nchini ambaye pia ni Mkuu wa Arusha, John Mongella, alisema, wamejipanga kutekeleza maelekezo ya Serikali.

"Mhe Waziri, sisi ni Wasaidizi wa Mhe. Rais, hii ajenda ameibeba mwenyewe Rais, kwa kuanza kuchanja, na sisi wengine baada yakuona amechanja, Wakuu wa Mikoa wote tukachanja, hii ni kuonesha kuunga mkono mapambano haya" alisema Mongela. 

Naye Prof. Riziki Shemdoe, Katibu Mkuu Tamisemi,  akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI,  Ummy Mwalimu, alisema, Mpango Harakishi na Shirikishi ni Mpango unaosimamiwa na Wizara zote ndio maana katika Kampeni hiyo wanashirikiana pamoja hasa ikizingatiwa kuwa Wizara hiyo ndio iliyo karibu zaidi na Wananchi.

Akitoa Salaam za Kamati ya Bunge, Mwenyekiti, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi Mhe. Fatma Tofiq, amesema wanaihakikishia Serikali, kuwa bega kwa bega katika kusukuma ajenda ya Chanjo. Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii Mhe. Dkt. Stanslaus Nyongo amempongeza Wizara ya Afya kwa namna ilivyoweza kutekeleza Maekezo ya Serikali pamoja na yale ya Bunge

"Mhe. Waziri kwaniaba ya Kamati ya Bunge, niwapongeze sana kwa jinsi mnavyotekeleza Maelekezo ya Bunge, lakini pia ya Serikali, niahidi kwaniaba ya Kamati kuendelea kukupa Ushirikiano wakati wote na kuwashauri inavyopaswa" Alisema Mhe. Nyongo.

Katika Hafla.hiyo, Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima aliitaja Mikoa vinara kwa Chanjo yaani iliyofanya vizuri katika Chanjo mpaka sasa kuwa ni Ruvuma, Mwanza, Dodoma, Kagera na Mara. huku akiitaka Mikoa mingine kuongeza bidii

Mwisho