Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAUGUZI MSINGI WA HUDUMA BORA ZA AFYA: DKT. MOLLEL

Posted on: May 21st, 2024


Na WAF, Tanga


Serikali kupitia Wizara ya Afya, imewapongeza Wauguzi nchini kwa kujitoa na utayari wao wa kutoa huduma bora, zenye staha na zinazojali utu.


Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 12, 2024 Jijini Tanga na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati wa maadhimisho ya siku ya Wauguzi Duniani ambapo Naibu Waziri Mkuu Dkt Dotto Biteko amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.


Dkt.Mollel ambaye pia ni Mbunge wa Siha amesema katika siku hiyo maalum ya kusheherekea siku ya Wauguzi Duniani, wanatambua na kusherehekea mafanikio makubwa ya wauguzi.


Pia amethibitisha dhamira ya Serikali kufanya kazi pamoja ili kujenga mustakabali wenye afya na usawa zaidi kwa wote.


 “Tunasema asante kwa wauguzi kwa kujitoa kwenu na utayari wenu wa kutoa huduma bora zenye staha na zinazojali utu”amesema Dkt.Mollel 


Hata hivyo amewasihi Wauguzi nchini waendelee kuwahudumia wateja kwa kuzingatia miiko ya taaluma yao.


"Huku mkitambua wajibu mlio nao katika kuimarisha afya za watanzania.Nawapongeza sana wauguzi wote wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri mnazofanya,"amesema Dkt.Mollel 


Mwisho