Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATUMISHI WAMETAKIWA KUSHIRIKIANA ILI KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI

Posted on: February 24th, 2024



Na WAF - Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amewataka watumishi katika sekta ya Afya nchini kufanya kazi kama timu na kudumisha ushirikiano ili kuzidi kuimarisha na kuongeza ufanisi na tija katika utoaji wa huduma bora kwa Watanzania.

Dkt. Jingu ameyasema hayo leo tarehe 24, 2024 jijini Dodoma wakati wa ziara yake ya kikazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma ili kukagua utendaji kazi na kuzungumza na watumishi wa hospitali hiyo ambapo ameambatana na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu na Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Best Magoma.

“Kwenye timu kuna namba tofauti tofauti, hapa tuna madaktari, wauguzi, wahudumu, watu wa utawala kila mmoja ana jukumu lake, tufanye kazi kama timu maana hii Hospitali yetu hata kama ina rasilimali nzuri kiasi gani kama hamfanyi kazi kama timu basi hamtaweza kufanya vizuri. Amesema Dkt. Jingu.

Dkt. Jingu ameelekeza Hospitali, zahanati na vituo vya kutolea huduma za afya nchini kuimarisha huduma kwa mteja na kuunda mfumo wa dawati la kusikiliza maoni, kero na malalamiko kwa wateja na kuwa na watoa huduma wenye weledi wenye kutumia lugha nzuri za staha pamoja na kulinda na kuzingatia haki za wagonjwa ikiwemo kutunza siri za wagonjwa .

Ni jukumu la kila mtumishi kuwahudumia wagonjwa sawa sawa kwa sababu tunategemea kila anaekuja kupata huduma ni mgonjwa hivyo huenda akawa na hasira ila unatakiwa kumuhudumia na kumpokea vizuri na nilitoa maelekezo kwa Hospitali zetu zote kuanzishwa kwa dawati la kusikiliza maoni, kero na malalamiko ya wateja ambalo linaonekana na kufikika na watoa huduma muda wote na wenye weledi na watakao kuwa na lugha za staha zinazozingatia mila na desturi zetu za kitanzania ikiwemo kutunza siri za wagonjwa". Amesema Dkt. Jingu.

Dkt. Jingu amepongeza watumishi wa Hospitali hiyo kwa ubunifu wa utoaji wa huduma bora na nzuri wagonjwa, usafi wa mazingira ya hospitali na ushirikiano walioutoa wakati wa janga la maporomoko ya Wilaya ya Hanang.

”Niwapongeze kwa ubunifu mlioufanya katika kila kitengo kuhakikisha huduma zote zinapatikana na kujitosheleza".