Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATUMISHI WA AFYA WAKIWA KUJIFUNZA MBINU MPYA KUTOKA KWA MADAKTARI BIGWA WA RAIS SAMIA

Posted on: June 24th, 2024

.

Na WAF - Geita

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Ndugu Herman P. Matemu, ametoa rai kwa watumishi wa Hospitali za kila Halmashauri za mkoa huo kutumia fursa ya kujengewa uwezo pamoja na uwepo wa madaktari bingwa wa Rais Samia kujifunza mbinu mpya ili baadae waweze kusaidia wananchi wenye matatizo mbalimbali ya kiafya.

Matemu ameyasema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe.Martine Shigela akiwapokea madaktari bingwa wa Rais Samia 35 mapema leo tarehe 24 Juni, 2024 katika Ofisi ya ya mkuu wa mkoa wa Geita.

“Uwepo wa madaktari bingwa hawa katika hospitali zote za Halmashauri zetu katika mkoa wetu ni fursa nzuri sana kwa wataalamu wetu kujifunza mbinu mpya za utoaji wa huduma za matibabu pasipo kwenda kujifunza mbinu hizo nje ya maeneo ya kazi. Hivyo, natoa rai kwa wataalam wetu wote watakaoshirikiana moja kwa moja na mabingwa hawa katika utoaji wa huduma, kutumia nafasi hiyo kujifunza kutoka kwao ili hata watakapoondoka mbakie na ujuzi wa kuwahudumia wananchi wetu” Amesema Matemu

Aidha, Matemu amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi na kufanyiwa uchunguzi ili wapate huduma bora kwa kuwa huduma hizi zinapatikana mbali na maeneo yao kwa gharama kubwa, ila Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasogezea Madaktari Bingwa karibu.

Naye Mganga mkuu wa Mkoa wa Geita Dkt. Omary Sukari amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeona umehimu wa kupeleka huduma za madaktari bingwa karibu na wananchi ili wapate huduma hizo kwenye maeneo yao pasipo kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo hii ni fursa muhimu sana kwa wananchi wa mkoa wa Geita kuchangamkia fursa hii adimu.

kwa upande wake Muwakilishi kutoka Wizara ya Afya Bi. Grace Mariki ameeleza kuwa, toka kambi za Madaktari bingwa wa Rais Samia kuanza kumekuwa na mwitikio mkubwa sana wa wananchi ambapo wananchi wamenufaika na hizi kambi za Madaktari Bingwa katika mikoa yote 26.

“Hadi kufikia wiki hii ya mwisho kila Serikali kupitia Wizara ya Afya imehakikisha kila Hospitali ya Halmashauri imefikiwa na hizi kambi haya ni mafanikio makubwa ya Rais Samia kupitia Wizara ya Afya na TAMISEMI kwa kufanikisha kuratibu kambi hizi kwa ufanisi ambpo lengo la kambi hizi ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kuwajengea uwezo Watumishi wa Afya katika kila Hospitali za Halmashauri za wilaya ili Kuboresha huduma za afya katika vituo vya ngazi ya chini vya kutolea huduma za Afya.

Mwisho.