Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATUMISHI SIMAMIENI SHERIA NDOGO NDOGO ZA SERIKALI ZA MITAA ILI KUKABILIANA NA KIPINDUPINDU

Posted on: January 24th, 2024

NA: WAF, Mwanza

Watumishi Sekta ya Afya wametakiwa kuhakikisha wanasimamia vyema sheria ndogondogo za serikali za mitaa katika kukabiliana na Ugonjwa wa Kipindupindu ili kuhakikisha afya ya jamii inaimarishwa na kuzingatiwa.

Hayo yamesemwa leo Januari 24, 2024 Mkoani Mwanza na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu wakati wa kikao na Watumishi na wadau sekta ya Afya katika kujadili juhudi na mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo.

“Niwasisitize viongozi wenzangu juu ya dhamana tuliyopewa ya kuhakikisha Afya za watu zinaimarika vyema, hivyo ni wajibu wetu kuweza kusimamia misingi na mikakati tuliyoweka katika kuhakikisha wananchi wanakua salama”. Amesema Prof. Nagu.

Aidha Prof. Nagu amesisitiza unawaji wa mikono kwa kutumia maji tiririka yaliyo safi na Salama Pamoja na kuzingatia hali ya usafi katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amoss Makalla amewataka wafanyabiashara wote kuzingatia kanuni za Afya katika maeneo yao ya biashara ili kuweza kuudhibiti ugonjwa huu.

Pia, Mhe. Makalla amelitaka Shirika linaloshughulikia masuala ya Barabara Vijijini na Mijini kuongeza kasi ya kusafisha mitaro na kuwakinga watumishi wanaosafisha mitaro kwa kuwapatia vifaa wezeshi kwa ajili ya kusafisha mitaro na kuondoa maji yaliyotuama.

Serikali imeendelea kufanya juhudi za kukabiliana na Ugonjwa wa Kipindupindu katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga kwa kupeleka Vifaa tiba na Dawa ya kutibu maji takriban million saba ili kuendelea kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu nchini.