Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATOA HUDUMA ZA AFYA NCHINI WATAKIWA KUTOA HUDUMA BORA KWA MATARAJIO YA WANANCHI

Posted on: July 14th, 2023

Na. Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam

Serkali kupitia Wizara ya Afya, imewataka watoa huduma za afya nchini kuanzia ngazi ya jamii mpaka Hospitali ya Taifa kuweka mikakati ya kutoa huduma bora na zinazokidhi matarajio ya wananchi kwa wakati kwa kutumia lugha yenye staha na unyenyekevu kitu kitakachowafanya waone matunda ya uwekezaji wa Serikali yao.

Wito huo ulitolewa Jijini Dar Es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe wakati alipokutana na Wakurugenzi Watendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili-MOI ili kujadiliana namna ya kuendelea kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa na hospitali hizo.

Dkt. Shekalaghe alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa ambao umehusisha ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya, hospitali za wilaya, Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Rufaa za Kanda, kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa, ununuzi wa vifaa tiba na kuajiri watalaamu wenye weledi wa kada mbalimbali za afya.

Alisema kuwa Wananchi wanategemea huduma bora wanapofika hospitalini kupata huduma za afya kwani serikali imetekeleza wajibu wake kwa kuboresha miundombinu na kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana katika hospitali zote

“Niwapongeze sana viongozi kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali imekuwa ikijivunia huduma zenu, hizi hospitali ndio taswira ya taifa katika utoaji wa huduma hivyo ninyi mkifanya vibaya mnaharibu taswira ya nchi nzima” alisema Dkt. Shekalaghe

Vile vile, aliwataka viongozi hao kuendelea kuzijengea uwezo Hospitali za Rufaa za Mikoa katika mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa zina vifaa tiba, mashine za uchunguzi na wataalamu kitu kitakachosaidia kupunguza msongamano katika hospitali hizi na zenyewe ziweze kujikita katika huduma za kibingwa na ubingwa bobezi.

Aidha, Dkt. Shekalaghe alitoa rai kwa wananchi kufuata ushauri wa wataalamu wa afya pale wanapopewa maelekezo kwa kuwa wataalamu hao wana weledi wa kutosha na ushauri wao huwa unazingatia taratibu za kiafya.

Mwisho, kikao hicho kiliwashirikisha Wakurugenzi wa taasisi hizo, Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya Prof. Paschal Rugajo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili Prof. Appolinary Kamuhabwa.