Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAMU WA KUTIBU SARATANI WATAKIWA KUJIKITA KATIKA KUFANYA TAFITI

Posted on: September 8th, 2023

Wataalamu wa Magonjwa ya Saratani nchini wametakiwa kujikita katika kufanya tafiti za kisayansi zitazowezesha nchi kuwa na teknolojia na ubunifu utakaosaidia utoaji wa huduma hususani za saratani.


Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa Wizara ya Afya Prof. Pascal Ruggajo ambaye alimwakilisha Waziri wa Afya katika kongamano la pili la kisayansi la magonjwa ya Saratani linaloendelea jijini Dar es Salaam.



Prof. Ruggajo amesema kuwa kwa sasa tunahitaji majibu ya changamoto zetu yatokane na sisi wenyewe.


"Takwimu zinaonyesha kwamba wagonjwa wapya wa saratani elfu 40 hugundulika kila mwaka huku vifo vinavyohusishwa na saratani vikifikia elfu 27 kila mwaka hivyo ni dhahili tunahitaji kutafakari kwa kina na kuweka mikakati ya pamoja kama taifa" ameeleza Prof. Ruggajo


Amesema wakati wa tatizo la UVIKO-19 kila taifa lilijaribu kutumia rasilimali za ndani kuokoa watu wake hivyo ni muda umefika sasa wa tupate majibu ya kisayansi yatakayowezesha kuunda nyenzo na matumizi ya dawa ikiwemo tiba asili za mwafrika ambazo zinaonyesha kutoa matumaini katika matibabu ya saratani. 


Aidha Prof. Ruggajo ameagiza kuwa bodi za kujadili wagonjwa wa saratani "Tumor Board" ziimarishwe na maamuzi ya bodi hizo yaheshimiwe kwa kuwa matibabu ya Saratani yanahusisha kada zaidi ya moja


Kwa Upande wake rais wa chama cha Madaktari wa Saratani Tanzania (TOS) Dkt. Jerry Ndumbalo amesema kuwa mkutano wa pili wa wataalamu wa Saratani unalenga kuwaleta pamoja wataalamu mbalimbali wanaohusika kutibu saratani kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kujadili jinsi ya kugundua saratani, kutibu kwa teknolojia mpya na kukinga.


"Mkutano huu umebeba kaulimbiu isemayo kuziba pengo katika utoaji wa huduma za saratani inayolenga kubainisha maeneo yenye upungufu katika utoaji wa huduma na kuyatafutia ufumbuzi" amesema Dkt. Ndumbalo