WATAALAM, WASIMAMIZI NA WATOA HUDUMAZA AFYA ZINGATIENI VIAPO VYA TAALUMA NA WELEDI.
Posted on: November 15th, 2023Na WAF, Morogoro
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amewataka wasimamizi na watoa huduma za afya nchini kote kuhakikisha wanatoa huduma kwa kuzingatia viapo vya taaluma zao, maadili ya kazi na weledi katika kuwahudumia wagonjwa ili kuokoa maisha ya watanzania na taifa kuwa na afya bora kwa ujumla
Dkt. Jingu ametoa wito huo wakati akizungumza na watumishi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ambapo amesema serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote wawatakao kiuka taratibu na kanuni za kazi kwani wanakwamisha jitihada za serikali ya awamu ya sita katika kuendelea kuboresha huduma za afya watanzania.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lengo letu kubwa kuokoa, kulinda maisha, kuleta unafuu na ahueni kwa wanaoteseka na magonjwa mbalimbali, kama daktari au muuguzi unajua miiko yako ya kazi ni ipi ili kufanya kazi kwa kuzingatia viapo vya taaluma zenu ili kuleta tija kwa wananchi kupata huduma bora", amesisitiza Dkt. Jingu.
Pia Dkt. Jingu amewataka wahudumu na wasimamizi hao kutambua umuhimu wa jukumu ambalo wamekabidhiwa ili kuweza kufikia malengo ya serikali katika kuwahudumia wananchi
Aidha Dkt Jingu amesema Serikali haitasita kumchukulia hatua msimamizi au mtoa huduma za Afya yoyote ambaye ataonekana kukiuka viapo vya taaluma na maadili ya kazi
“Serikali haya mambo hatuwezi kuyavumilia lazima tuyashughulikie kwa nguvu zote za kisheria, kwa kuchukua hatua kali kwa wote wanaofanya uzembe kwa sababu kosa moja dogo tu linaweza kuasababisha mtu kupoteza maisha ama mtu kupata kilema cha kudumu, Kwahiyo ni lazima tufanye kazi kwa kuzingatia maadili na tusikubali uzembe upite kati yetu” ameongeza Dkt. Jingu
Naye Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewashukuru na kuwapongezi watoa huduma za afya katika Hospitali kwa kutambua kazi kubwa wanayoifanya ya kuwahudumia watanzania ili kuwa na taifa lenye afya bora.