Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAM WA AFYA WATAKAIWA KUTUMIA UWEKEZAJI KUTOA HUDUMA KWA UFANISI NA TIJA.

Posted on: May 15th, 2024



Na WAF - Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu amewataka wataalamu wa Afya Nchini kutumia uwekezaji Mkubwa unaofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika Hospitali za Rufaa nchini ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala kuwezesha utoaji wa huduma kwa urahisi na ufanisi kwa kuzingatia tija inayotakikana.

Dkt.Jingu amebainisha hayo Mei 5, 2024 akiwa Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kuangalia utekelezaji wa miradi iliyopo Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala Jijini Dar Es Salaam na kuangalia hali ya utoaji wa Huduma inavyondelea.

Amesema Mapinduzi Makubwa ya uboreshaji wa huduma yanayofanyika katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala lengo la Serikali ni nikuongeza ufanisi kwa watoa huduma.

"Hospitali zetu zina vifaa vizuri vya utoaji wa huduma, vikubwa kwa vidogo ambavyo vinawezesha wataalamu wetu kuto huduma zenye matokeo yanayotakiwa, Mtu akija Hospitali anataka apate matokeo anayoyataka maanake kupata matibabu bora kulingana na changamoto aliyonayo" amesema Dkt. Jingu.

Dkt Jingu ameongeza kuwa katika kufanikisha hilo Wizara ya Afya imeweka Miundombinu Mbalimbali ili kurahisisha utowaji wa huduma kwa kuzingatia mapinduzi ya Teknolojia.

"Teknolojia na Tehama zinatusaidia sana sasa hata vituo vya afya na hata Zahanati na zenyewe zinaanza kutoa huduma kwa weledi Mkubwa zaidi Sasa hivi, kuna kitu tunakiita Telemedicine hii ni tiba mtandao, wataalamu wetu sasa wanaweza kushirikiana na wenzao waliopo Hospitali kubwa zaidi wanaweza kusaidiana kutatua changamoto yoyote ambayo wanaiona kwa kubanadilisha maarifa na huduma zikawa nzuri sana" ameongeza Dkt. Jingu
Dkt. Jingu amesema pia Katika kuzidi kuboresha Sekta ya Afya kuwa na huduma zinaondana na uwekezaji unaofanya na Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara inaendelea kuboresha Mifumo ya Mawasiliano hasa huduma kwa wateja Baina ya Mgonjwa na Mtoa huduma.