Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WATAALAM WA AFYA NGAZI YA MSINGI WAKUMBUSHWA UWAJIBIKAJI KAZINI

Posted on: February 13th, 2024


Na WAF - Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe amewataka Madaktari, Wauguzi, Wataalamu wa maabara na Wataalamu wote wa afya kuwa na utaratibu wa kupita maeneo ya huduma kuangalia wananchi wanavyopata huduma ikiwemo kuangalia muda wanaokaa na kusubiri kupata huduma badala ya kukaa ofisini.

Dkt. Magembe ametoa maelekezo hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waganga wafawidhi kabla ya ufunguzi wa Mkutano wa kwanza wa mwaka kwa waganga wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za Afya ya msingi nchini.

"Nasisitiza daktari, muuguzi, mtaalamu wa maabara na wengine wote piteni mawodini na kufungua majalada ya wagonjwa kuona huduma gani wagonjwa wamepatiwa tangu wamefika hospitali, je wanapata dawa na vipimo vilivyoandikwa, watumishi wapo na kama wanawajibika”. Amesisitiza Dkt. Magembe.

Ameongeza kwa kusema kuwa watumishi wasijifungie maofisini tu, bali watumie ujuzi wao kama viongozi wa vituo kuhakikisha wanatoa Huduma bora kwa wananchi ili kuleta thamani ya uwekezaji wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya nchini.


"Kama wananchi watafika mahali hawaoni tofauti ya ukiwepo na usiwepo basi wewe kitaaluma ni mfu maana taaluma yako haigusi maisha ya watu". Amesema Dkt. Magembe.
Hata hivyo amewataka waganga hao kuimarisha ushirikiano wao na watumishi wanao waongoza ili kuleta ubora wa huduma katika kuwahudumia wananchi.

Aidha, Mkutano huo ulenga kuboresha uwajibikaji katika kutoa huduma bora za Afya ya msingi kwa Watanzania ili kila mwananchi anufaike na uwekezaji uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Afya nchini.

Mkutano huo umebebwa na kaulimbiu "Uwajibikaji ni nguzo muhimu katika utoaji wa huduma bora za Afya ya msingi"