WASANII KUWA MABALOZI WA KUELIMISHA UKIMWI
Posted on: October 16th, 2023
Na. WAF - Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya imewasihi wasanii kutumia maarifa yao kuandaa kazi ya sanaa yenye jumbe sahihi iliyochanganyika na burudani ya kusisimua wakati ikitoa elimu kuhusu VVU na UKIMWI.
Rai hiyo imetolewa leo na Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI (NACP) Dkt. Aneth Rwebembera wakati akifungua semina elekezi ya VVU na UKIMWI kwa wasanii iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Ni dhahiri kuwa Sanaa imekuwa ikitumika katika kueleimisha jamii kuhusu magonjwa mbalimbali ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ni juhudi za wasanii wenyewe ingawa kwa nyakati tofauti, Serikali imekuwa ikiwashirikisha katika kampeni mbalimbali ni kwa sababu Serikali inatambua umuhimu wa tasnia ya Sanaa nchini”. Amesema Dkt. Rwebembera
Aidha, Dkt. Rwebembera amesema kuwa Tanzania imekuwa mojawapo ya nchi zenye mafanikio makubwa ambapo kufikia mwezi Machi 2023, inakadiriwa kuwa watu Mil. 1,729,408 wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) watu 1,631,968 sawa na 94.4% wanatambua hali yao ya maambukizi ambapo kati ya hao, 98.8% wako kwenye dawa za kufubaza VVU (ARVs) na 96.6% yao wamefikia kiwango cha chini cha VVU mwilini (Viral suppression)
Wakati akiendelea kuongea na wasanii hao Dkt. Rwebembera ametoa rai kwa watu wote wanaoishi na VVU (WAVIU) wapime na kutambua hali yao ya maambukizi na 95% ya watu waliopimwa na kugundulika na maambukizi ya VVU wawe wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU.
“Lakini pia asilimia hiyo 95 ya watu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya VVU wawe wameshusha na kufikia kiwango cha chini cha VVU mwilini (95 ya tatu) ili kufikia lengo la Serikali la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030”. Amesema Dkt. Rwebembera
Pia, Dkt. Rwebembera amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI imejipanga kutokomeza ugonjwa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030 nchini Tanzania.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo katika sekta ya afya, itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali Kwa lengo la kuzuia maambukizi ya VVU, matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs, pamoja na huduma za kupunguza gharama za matibabu ili kufikia malengo ya kimkakati ya dunia ya 95 tatu unaolenga kutokomeza maambukizi ya VVU na UKIMWI ifikapo mwaka 2030”. Amesema Dkt. Rwebembera