Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

Wasambazaji Maziwa mbadala na vyakula vya watoto zingatieni sheria

Posted on: August 2nd, 2022

Sekta binafsi, wasindikaji, wasambazaji na wauzaji wa  maziwa mbadala na vyakula vya watoto wameagizwa kuepuka matangazo ya bidhaa zao ili kuzingatia sheria na kanuni ya kudhibiti uuzaji na usambazaji wa maziwa na vyakula vya watoto wachanga na wadogo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Mhe. Mwanaidi Khamis wakati akiongea na wananchi wa  Halmashauri ya Ikungi, Mkoani Singida katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa watoto duniani.

"Mnapaswa kuzingatia Sheria na Kanuni ya Kudhibiti Uuzaji na Usambazaji wa Maziwa na Vyakula vya Watoto wachanga na wadogo kwa kuepuka utoaji wa matangazo, ushawishi na kufanya promosheni ya maziwa mbadala na vyakula vya watoto wachanga kwenye vyombo vya habari au katika maeneo yoyote".

Aidha, alisema   Viongozi wa kijamii wakiwemo Viongozi wa Dini na Siasa, watu maarufu wenye ushawishi katika jamii, wasanii na wanamichezo wana wajibu wa kuhamasisha jamii kuhusu unyonyeshaji wa maziwa ya mama".

Naibu Waziri huyo amewataka  wasambazaji na wasindikizaji wa maziwa mbadala na vyakula vya watoto kutafuta na kusambaza taarifa sahihi zinazohusu unyonyeshaji na lishe na kuepukua kusambaza taarifa au imani potofu zinazoathiri unyonyeshaji.

Hata hivyo ametoa rai kwa  sekta ya viwango na udhibiti ubora wa vyakula, wanataaluma na taasisi zinazosimamia sheria zinazohusu vyakula vya watoto kuendelea kufanya tafiti na ufuatiliaji wa kina wa taratibu za uuzaji na usambazaji wa maziwa na vyakula vya watoto wachanga na wadogo ili kusaidia kuwalinda watoto hao dhidi ya athari wanazoweza kuzipata kutokana na kutumia bidhaa zisizokuwa na ubora na pia kulinda na kuendeleza unyonyeshaji watoto maziwa ya mama.

"Ujumbe wa wiki ya unyonyeshaji mwaka huu inayosema "Chukua hatua endelez unyonyeshaji, Elimisha na toa msaada" unatukumbusha sote tuna wajibu wa kuwawezesha wanawake waweze kunyonyesha watoto wao maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo baada ya kujifungua".

Wakati huohuo Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Victoriana Ludovick amesema asilimia 93.4 ya akina mama na walezi katika Mkoa huo wamepatiwa elimu ya unyonyeshaji pia moja ya mikakati ya Mkoa ni suala la lishe kupewa kipaumbele na shughuli za lishe zinajumuishwa kwenye mpango kabambe wa Halmashauri.