WANANCHI ZAIDI YA 4000 WAPATA HUDUMA YA ULTRA SOUND, X-RAY, HOSPITALI YA WILAYA SONGWE
Posted on: August 12th, 2024
Na WAF - Songwe.
Wananchi wapatao 4870 wamepatiwa huduma za Ultrasound ikiwemo wajawazito katika Hospitali ya Wilaya ya Songwe ikiwa ni miaka mitatu tangu kuanza rasmi kutoa huduma kwa Hospitali hiyo hali iliyo kupunguza rufaa kwa wagonjwa.
Hayo yamebainishwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Ntufye Kapesa wakati akielezea hali ya utoaji wa huduma za matibabu kwenye hospitali hiyo.
"Mashine za UltraSound zilizopo ni za kisasa na zinatoa huduma kwa wamama wajawazito na huduma zingine zinazohitajika lakini pia zinauwezo wa kutoa majibu ya papo kwa papo kwa njia ya simu ya mkononi. Amesema Dkt. Ntufye
Dkt. Ntufye amesema mbali ya Utrasound vilevile hospitali imekuwa ikitoa huduma za mionzi (X-Ray) ambapo imeweza kuwahudumia wangonjwa zaidi ya 1760.
“Kati ya wangonjwa waliopatiwa matibabu ya X- Ray wengi wao wakiwa ni waliopata ajali na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.” Amesema Dkt. Ntufye.
Katika hatua nyingine Dkt. Ntufye amesema kuwa, Hospitali ya Wilaya ya Songwe kupitia jengo la dharura lenye vifaa vya kisasa lililoanza kutoa huduma toka Oktoba, 2023 limeweza kuhudumia wagonjwa 890 wa dharura hadi sasa.
“Jengo la Dharura linahudumia wagonjwa wa ajali pamoja na wagonjwa wengine wanaohitaji huduma za dharura na lina vifaa vyote vya kisasa" amefafanua Dkt. Ntufye
Dkt. Ntufye ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kupeleka watumishi kwenda kusoma na kujifunza namna ya kutumia vifaa hivyo.