Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WANANCHI WATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI KUKABILIANA NA UGONJWA WA KIPINDUPINDU

Posted on: January 23rd, 2024


NA; WAF, Shinyanga.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kufanya usafi na kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo Pamoja na kunywa maji safi na salama ili kuepukana na ugonjwa wa Kipindupindu.

Hayo ameyasema leo Januari 23, 2024 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Igumilo Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga mara baada ya kukagua chanzo kinachosadikika kuwa chanzo cha ugonjwa huo ambao ni Mto Tungu.

“Niwaombe wananchi kuzingatia usafi na kwa mgonjwa yeyote yule ambao ana dalili za ugonjwa huu ikiwa ni kutapika na kuharisha basi awaishwe kwenye kituo cha afya na mtoe taarifa kwa viongozi ili hatua za haraka zichukuliwe”. Amesema Prof. Nagu.

Aidha Prof. Nagu amesema kila wananchi anawajibu wa kulinda afya yake na familia yake kuwakinga na madhara Pamoja na mlipuko huu wa kipindupindu kwa kutumia maji safi na salama kwa kuyatibu na dawa au kuchemsha na kuhifadhi sehemu iliyo salama.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Christina Mndeme amehimiza matumizi sahihi ya vyoo na kuwataka wananchi wote wazingatie usafi wa mazingira ili kuendelea kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu usiendelee.

Mhe. Mndeme amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Kipindupindu na kufuata ushauri wa wataalamu katika kukabiliana na ugonjwa huu.

Hata hivyo amewataka watendaji wa kata kuhakikisha wananchi wote wanatumia vyoo na yule atakaebainika hana choo katika kaya yake awajibishwe kisheria.