WANANCHI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KWA WINGI KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA RAIS DKT. SAMIA MKOANI MBEYA
Posted on: September 16th, 2025
Na WAF, Mbeya
Wananchi zaidi 2,500 wanatazamia kupatiwa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika mkoa wa Mbeya kupitia kambi maalum ya Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia, inayoanza wiki hii mkoani humo na kwenda kwa siku sita (6) .
Huduma hizo, zinazoratibiwa na Wizara ya Afya, zinalenga kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao na kupunguza gharama na usumbufu wa kufuata matibabu mbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu nyingine ya huduma hizo leo Septemba 15, 2025 Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma hizo adhimu.
“Hii ni fursa ya kipekee kwa wananchi wetu. Tuitumie kama dhahabu. Huduma hizi ni za kibingwa na zinapatikana karibu kabisa na maeneo tunayoishi, Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia kwa moyo wake wa kizalendo na kuonesha upendo wa dhati kwa wananchi wake,” amesema Mhe. Malisa.
Aidha, Mhe. Malisa amepongeza Wizara ya Afya kwa uratibu mzuri wa huduma hizo pamoja na wataalamu wa afya waliotoa huduma kwa kujitolea kwa siku za nyuma akiamini pia awamu hii itakuwa ya mafanikio.
Kwa upande wake, Mratibu wa huduma hizo, Bw. Ulimbakisye Macdonald, ameeleza kuwa tangu kuanza kwa mpango huo kitaifa Mei 2024, jumla ya wananchi 230,532 wamehudumiwa kote nchini.
“Idadi hii inaonyesha ni kwa kiasi gani huduma hizi zimekuwa mkombozi kwa Watanzania wengi, Wataalamu wetu mabingwa na mabobezi wamekuwa wakijitoa kwa moyo mmoja kuhudumia wananchi,” amesema Bw. Macdonald.
Madaktari Bingwa wanaoshiriki katika huduma hizo, akiwemo Dkt. Anna Magembe kutoka Hospitali ya Kanda – Mbeya na Dkt. Catherine Mdemu, Muuguzi Bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa, wameeleza kuwa wamejipanga kikamilifu kutoa huduma bora huku Wakiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi ili kufaidika na uwepo wao.
“Tupo tayari kuwahudumia. Wananchi wajitokeze kwa wingi ili tuwasaidie kupata suluhisho la matatizo yao ya kiafya,” wamesema kwa pamoja.
Huduma hizi zinaendelea kutolewa katika hospitali zote za halmashauri Jijini Mbeya, zikiwa ni sehemu ya jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa Watanzania wote, hasa walioko pembezoni.