WANANCHI SHINYANGA WATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI KUPATA HUDUMA ZA KIBINGWA NA BOBEZI
Posted on: October 13th, 2025
NA WAF – SHINYANGA
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewahimiza wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kufuata huduma za afya za kibingwa na bobezi, kufuatia ujio wa timu ya madaktari bingwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan waliotia kambi katika mkoa huo, wakitoa huduma katika hospitali za halmashauri zote za mkoa huo.
Akizungumza leo, Oktoba 13, 2025, ofisini kwake wakati akiwakaribisha Madaktari hao, Mhe. Mhita amesema kuwa mkoa wa Shinyanga umefarijika sana kwa uwepo wa madaktari bingwa, kwani ni fursa kubwa kwa wananchi kupata huduma bora za afya.
“Hii ni awamu ya nne tunapokea madaktari bingwa na bobezi, ambapo wanaendelea kusogeza huduma kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali, sambamba na kuwajengea uwezo na ujuzi wataalam wa afya wa mkoa wetu,” amesema Mhe. Mhita.
Ameongeza kuwa huduma hizo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wengi wenye changamoto za kiafya na zimechangia kuongeza uelewa kuhusu afya bora miongoni mwa jamii ya Shinyanga.
“Huduma za kibingwa zinapunguza gharama za matibabu kwa wananchi, lakini pia zinawapatia uelewa wa kitaalam na kuwaondoa kwenye imani potofu za kishirikina kuhusu magonjwa yanayojitokeza katika jamii,” amesema Mhe. Mhita.
Aidha, Mhe. Mhita amesema jitihada hizo ni sehemu ya kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuimarisha sekta ya afya nchini na kusogeza huduma za kibingwa na bobezi kwa wananchi wote.
Amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata huduma za kibingwa na bobezi na kuondokana na gharama zisizo za lazima.