WAKUU WA IDARA WA HOSPITALI WATAKIWA KUWEKA MKAKATI WA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA
Posted on: February 6th, 2022Wakuu wa Idara wa hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwl.JK Nyerere wametakiwa kuweka mkakati wa kuboresha huduma za afya kwenye hospitali hiyo.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi wakati akiongea na watumishi wa hospitali hiyo kwenye kikao cha pamoja ikiwa ni siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuitembelea hospitali hiyo.
Prof. Makubi amesema kuwa ni wakati sasa wa wakuu hao wa idara kukaa na kujitathimini ili kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuboresha huduma za hospitali hiyo kwani watu wanafuata huduma bora"lazima muanze vizuri,mfanye kazi ili msije kuiangusha nyota mliyoletewa na Rais,fanyani kazi kwa bidii kwani mpo kwenye fani sahihi".
Ameongeza kuwa wakuu hao wa idara wanatakiwa wabebe majukumu yao, watumishi wajitambue,wabadilike kifikra ili hospitali iweze kwenda mbele kwenye utoaji wa huduma.
Hata hivyo Prof.Makubi hakusita kuwakumbusha watumishi wa chini kufanya kazi kwa kujituma,kubadilika na kuwa walinzi wa mali zilizopo kwenye hospitali hiyo na siyo kusubiri wakaguzi kutoka nje .
"Huduma nzuri inaanzia getini,kujiandikisha na kila eneo,kuweni na lugha nzuri,jipimeni kwa kutumia muda mfupi kwa wagonjwa,mgonjwa afanyiwe vipimo vinavyohitajika,shikamaneni ili tuimalize hospitali hii"Alisisitiza Prof. Makubi
Vile vile Katibu Mkuu huyo hakusita kuwasisitiza watumishi hao kusimamia mapato ya hospitali hiyo ili kuboresha huduma za hospitali hiyo na hata kwa wao wenyewe watapata motisha na kuongeza morali ya kufanya kazi.