Wizara Ya Afya

WAKUFUNZI CHUO CHA AFYA MVUMI WATAKIWA KUZINGATIA MBINU ZA KISASA KWENYE MAFUNZO KADA ZA AFYA

Posted on: July 13th, 2026

Na Atley Kuni, WAF-Dodoma

Wakufunzi wa Chuo cha Afya Mvumi wametakiwa kuzingatia mafunzo maalum yanayotolewa na wizara ya afya kuhusu afya ya uzazi ili waweze kuendana na mahitaji ya sasa, hatua itakayo wezesha kuokoa uhai wa mama na mtoto.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Mafunzo hayo kutoka Wizara ya Afya Bi. Notgera Ngaponda, leo Julai 13, 2026 wakati akifungua rasmi mafunzo ya wakufunzi wa afya ya uzazi, mama na mtoto kwa Mkoa wa Dodoma yanayofanyika katika Chuo cha Afya Mvumi, yakihusisha wakufunzi 12 wa chuo hicho.

Bi. Ngaponda amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kuweka kipaumbele kuimarisha uwezo wa rasilimali watu ili kuhakikisha huduma za afya zinazotolewa nchini zinakuwa bora, salama na zenye kuzingatia Utu , heshima na viwango kwa mujibu wa miongozo ya kitaifa na kimataifa.

"Ubora wa huduma za afya huanza na ubora wa mafunzo yanayotolewa kwa wataalamu wa afya, hivyo wakufunzi wana nafasi ya kipekee ya kuzalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi na maadili yatakayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi," amesema Bi. Ngaponda.

Bi. Ngaponda amewataka washiriki kutumia mafunzo hayo kama fursa ya kuimarisha maarifa, kujifunza mbinu mpya za ufundishaji na kubadilishana uzoefu.

Amewahimiza washiriki kushiriki kikamilifu mijadala na kazi za vitendo zitakazowasilishwa wakati wa mafunzo, akisisitiza kuwa maarifa watakayoyapata ni tathmini ya kitaifa iliyofanyika mwaka uliopita.

Katika hatua nyingine Notgera amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya sekta ya afya kupitia mafunzo ya mara kwa mara kwa wakufunzi na watumishi wa afya, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha ubora wa huduma za afya.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameeleza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka, yakitarajiwa kuzidi kuwaboreshe majukumu yao ya kitaaluma kufundisha na kusimamia utoaji wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuendelea kwa siku mbili katika Chuo cha Afya Mvumi, Mkoa wa Dodoma, lakini pia yanatolewa kwenye vyuo vingine 47 vya kati na vya elimu ya juu nchi nzima vikiwahusisha wakufunzi 450.