Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAJAWAZITO MILIONI 1,607,540 WALIJIFUNGUA KATIKA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA MWAKA 2023/24 Na WAF - Dodoma

Posted on: May 14th, 2024

UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA YA AFYA 2023/24


Serikali kupitia Wizara ya Afya imebainisha kuwa kati ya Julai 2023 hadi Machi 2024, wajawazito Milioni 1,607,540 sawa na asilimia 97.85 walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema hayo Bungeni Mei 13, 2024 akiwa anawasilisha hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 akielezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika utoaji wa huduma za Kinga nchini.

Amesema, Julai 2022 hadi Machi 2023 wajawazito 1,504,384 ambao ni sawa na asilimia 97.75 walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, Waziri Ummy amesema kati ya Julai 2023 hadi Machi 2024, vituo vya Afya vilivyotoa huduma ya upasuaji kwa wajawazito (CEmONC centres) vilikuwa 525 ambapo kwa Mwaka 2022 hadi Machi 2023, vituo vilikuwa 475.

"Julai 2023 hadi Machi 2024 wajawazito Laki 188,885 ambao ni sawa na asilimia 11.65 ya wajawazito waliojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya walijifungua kwa njia ya upasuaji." Amesema Waziri Ummy

Mwisho, Waziri Ummy amesema ongezeko hilo linaendana na jitihada za Serikali kupeleka huduma hizi karibu na wananchi ili kuendelea kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.