WAHITIMU 3,561 WA MAFUNZO YA HUDUMA ZA AFYA NGAZI YA JAMII, WAPATIWA VITENDEA KAZI.
Posted on: September 8th, 2025
Na WAF- Lindi
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa OR-TAMISEMI kwa kushikiana na Wadau wa Sekta ya Afya imekabidhi seti ya vitendea kazi kwa Wahudumu wa Afya (WAJA) 3,561 waliohitimu mafunzo ya kutoa huduma za afya ngazi jamii.
Hayo yamejiri Septemba 08, 2025 kupitia hafla fupi ya utoaji wa vyeti kwa wahitimu 222 katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, wakiwakilisha kundi la Wahudumu 3,561 awamu ya kwanza ya wahudumu waliohitimu mafunzo hayo katika mikoa 12.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bi. Zuwena Omary Jiri, akizungumza kwenye hafla hiyo amesema Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya karibu zaidi na wananchi na sasa tunashuhudia wahudumu hawa wa afya ngazi ya jamii wamehitimu na wapo tayari kwa ajili ya kuanza kazi wakiwa na nyenzo zote muhimu kwa ajili ya kufanya kazi kwa ufanisi.
“Mpango huu ulizinduliwa mwaka 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Phillip Isdor Mpango, hapo nyuma katika miaka 1970 tulikuwa na mpango huu pia lakini ulipitia changamoto za uratibu na awamu hii programu hii ya WAJA imeboreshwa zaidi ili kuleta tija zaidi katika kuimarisha huduma za kinga ndani ya jamii ili kufikia lengo la Huduma za Afya kwa wote ifikapo mwaka 2030,” amesema Bi. Zuwena.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema Wahudumu hao huchaguliwa na wananchi katika maeneo yao wanayoishi ambapo kila kitongoji au mtaa huchagua watu wawili, mwanaume na mwanamke ambao Wizara huwapatia mafunzo ya darasani kwa muda wa miezi mitatu na miezi mitatu mafunzo kwa vitendo katika jamii.
“Wahudumu hawa wa afya wako tayari kwa ajili ya kwenda kutoa huduma katika jamii, na leo hii Serikali inatoa vitendea kazi ikiwemo, sare, baiskeli, vishikwambi (tablets) vifaatiba ikiwemo vifaa vya kupimia shinikizo la damu, sukari, joto, uzito na vipeperushi vya elimu ya afya, yote haya ikiwa ni kuhakikisha mnakwenda kusaidia katika kuiamarisha huduma za kinga ndani ya jamii,” amesema Dkt. Magembe