Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAHANDISI WA VIFAA TIBA NA WATAALAMU WA AFYA TUNZENI VIFAA KWA MAENDELEO YA SEKTA YA AFYA

Posted on: November 23rd, 2023

Na WAF – DODOMA

Wahandisi wa Vifaaa Tiba na wataalam wa afya Nchini wametakiwa kulinda na kutunza vifaa vya kisasa ambavyo Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza na kupunguza uhaba wa Vifaa vya huduma za Afya hapa nchini.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo Wizara ya Afya, Dkt. Saitore Laizer wakati akimuawakilisha Waziri wa Afya, katika ufunguzi wa Kongamano la pili la Wahandisi wa Vifaa Tiba, Novemba 23, 2023 Jijini Dodoma.

Dkt Laizer amesema utunzaji wa vifaa hivyo utasidia serikali kupunguza adha na gharama za Matengezo ya vifaa hivyo na fedha ambazo zingesaidia kuleta maendeleo kwenye kada nyingine.

“Wahandisi wa Vifaa Tiba mnatakiwa kuvilinda na kuvitunza kwasababu Serikali imewekeza na kuboresha miundombinu ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza kwa kununua vifaa tiba, kuvisimika na kutoa elimu kwa wataalam wa afya namna ya matumizi bora ya vifaa” aamesisitiza Dkt. Laizer

Dkt. Laizer ameongeza kuwa Serikali licha ya kuwekeza vifaa vya kisasa bado imeendelea kupunguza uhaba wa wataalamu, watoa huduma za Afya na wataalam wa kufanya matengenezo na kurabati mitambo ya Tiba.

“Katika kipindi cha 2021 na 2023 jumla ya wataalam zaidi ya 280 wa kada ya Uhandisi wa vifaa tiba wameajiriwa. kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza afua zenye lengo la kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa Sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na kujenga na kukarabati karakana za ufundi wa vifaa tiba na ununuzi wa vitendea kazi katika ngazi mbalimbali” ameeleza Dkt. Laizer

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amepongeza baadhi ya vyuo kwa kuona haja ya kuanzisha kozi ambazo zinamsaada katika Sekta ya Afya Nchini huku akisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kujiendeleza kielimu wataalam na Wahandisi wa Vifaa Tiba Nchini.