Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGONJWA ZAIDI YA 100 WAREJESHEWA UONO KAMBI YA MATIBABU YA UPASUAJI WA MTOTO WA JICHO.

Posted on: June 21st, 2024


Na WAF - Chunya, Mbeya

Wagonjwa zaidi ya 100 wamefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho kupitia Kambi ya siku saba ya Madaktari Bingwa wa Macho iliyowekwa katika hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.

Hayo yameelezwa na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. John Ndundumka Juni 21, 2024 wakati wa kampeni ya matibabu ya upasuaji wa mtoto wa jicho uliofadhiliwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Hellen Keller International.

Dkt. Ndundumka amesema lengo ni kufikia wagonjwa zaidi 450 ambao wanatarajiwa kuonwa kupitia kampeni hiyo ya matibabu ya upasuaji baada ya kufanyiwa vipimo vya awali ambapo wagonjwa hao wametoka katika kata 21 za wilaya ya Chunya.

“Kampeni hii haijawahi kutokea kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Chunya, ambapo wananchi wenye kipato cha chini wameweza kunufaika kwa kupata matibabu ya upasuji wa mtoto wa jicho, kawaida huduma hii inagharimu shilingi milioni moja na laki mbili hivyo mwananchi wa kawaida hawezi kumudu ila kupitia kambi hii anapatiwa matibabu bure”.

Kwa upande wake Afisa kutoka Wizara ya Afya kitengo cha Mpango wa Taifa huduma za macho Dkt. Greater Bruno Mande amesema Kipaumbele kimoja wapo cha Wizara ni kuendelea kuwafikishia huduma za Afya ya macho karibu zaidi na wananchi hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kutumia fursa ya uwepo wa kambi hizo katika maeneo yao kujua afya zao na kupatiwa matibabu.

“Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Hellen Keller International tayari imeshafanya kambi sita na inatarajia kufanya kambi nyingi zaidi hivyo amewataka wananchi wananchi kujitokeza kwa wingi pindi wanapopata taarifa ya uwepo wa kambi za matibabu katika mikoa yao”. Amesema Bruno.

Aidha, Dkt. Greater ameshukuru uongozi wa Wilaya ya Chunya kwa ushirikiano wanaoutoa kwenye kampeni hiyo na kuishukuru taasisi ya Hellen Keller Intl kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwasongezea huduma ya Matibabu ya Upasuaji wa Mtoto wa Jicho inayotolewa bure.