Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGONJWA 2,808 WAPATIWA HUDUMA BURE ZA MATIBABU YA KIBINGWA KONDOA

Posted on: October 12th, 2024

Na WaF Dodoma

Kambi ya matibabu ya kibingwa yenye jumla madaktari bingwa 27 wa kujitolea iliyoratibiwa na Taasisi inayojihusisha na kutoa huduma kwa wagonjwa na yatima (JAI) kwa kushirikiana na Amana Bank imetoa matibabu, dawa na uchunguzi wa kibingwa bure kwa wagonjwa 2,808 kwa siku tano (5), Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule tarehe 11 Oktoba, 2024 katika hafla ya kufunga kambi hiyo, iliyokuwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa Mji, mkoani Dodoma kuanzia tarehe 7 hadi 11 Oktoba, 2024.

"Sisi kama Mkoa wa Dodoma tutawakumbuka JAI kwa kazi nzuri na kubwa ambayo itabaki katika moyo ya watu hawa 2,808 waliopata huduma kila mtu atakumbuka huenda amepona kwa kazi nzuri na kubwa mmeyofanya," amesema Mhe. Senyamule.

Kwa upande wake kiongozi wa Madaktari Bingwa hao Dkt. Husein Msuma ambae ni Daktari Bingwa wa Upasuaji amesema, kwa ujumla kambi hiyo imefanikishwa na madaktari bingwa 26 wa kujitolea kutoka Tanzanja Bara na Zanzibar wakiwemo Madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani, wakina mama na Uzazi, upasuaji wa jumla na njia ya mkojo, magonjwa ya koo, pua na masikio, mifupa, watoto, afya ya akili, kinywa na meno, wataalam wa lishe, dawa, maabara na upimaji.

"lengo la kambi hii ni kutoa huduma za kibingwa za afya kwa jamii ya Watanzania ambao uwezo wao wa kuchangia huduma ni mdogo pia kuwajengea uwezo watoa huduma katika vituo vya vya kazi na kuhamasisha uchangiaji wa damu katika jamii," ameeleza Dkt. Msuma.