Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

Wagonjwa 150 kutibiwa mfumo wa fahamu na mifupa katika kambi ya BMH

Posted on: July 22nd, 2022

Wagonjwa wapatao 150 wanatarajiwa kupatiwa matibabu ya mfumo wa fahamu katika kambi ya siku tatu itakayofanywa na madaktari wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Hospitali ya Appolo ya nchini India.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kambi ya matibabu ya mfumo wa fahamu na upasuaji wa mifupa, Mkurugenzi wa mafunzo na utafiti wa BMH Bi. Monica Kessy amesema kambi hiyo itakua ya siku tatu na kati ya wagonjwa hao watapata matibabu ya mfumo wa fahamu pamoja na upasuaji wa mifupa.

Amesema Hospitali hiyo inafungua milango ya ushirikiano na hospitali nyingine za nje ya nchi ili kuendelea kuwajengea uwezo Madaktari wao katika taaluma mbalimbali.

"Hospitali ya Benjamin Mkapa inajiandaa kuwa Hospitali ya Taifa hivyo kuendelea kupata uzoefu kwa Hospitali zilizo tangulia itasaidia kutupatia uzoefu katika kuwahudumia wananchi" Alisema

Naye, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Mfumo wa Fahamu na Ubongo , Dkt. Henry Humba, amesema kambi hiyo ni muhimu kwa kuwa idadi ya wagonjwa wa mfumo wa fahamu na ubongo, upasuaji wa mifupa inazidi kuongezeka.

"Kambi hii ni muhimu kwa kuwa Idadi ya wagonjwa wa mfumo wa fahamu na ubongo, upasuaji wa mifupa imeongezeka dhidi ya uwiano wa madaktari bingwa wa magonjwa hayo" alisema.

Daktari Bingwa wa mfumo wa fahamu kutoka hospitali ya Apolo ya nchini India, Dkt. Mangaleswan Balamurugan amesema kambi hiyo ya pamoja, mbali na kuipunguzia mzigo BMH pia ni sehemu ya kubadilishana uzoefu baina ya madaktari wa nchi hizo mbili.

"Kambi hii ya pamoja ni muhimu kwa kuwa inatupa fursa ya kubadilishana uzoefu na wenzetu katika fani hii,"alisema Daktari Bingwa wa mfumo wa fahamu na ubongo kutoka Appolo ya India.