Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGANGA WAKUU WA WILAYA WATAKIWA KUIMARISHA MFUMO WA UFUTILIAJI WA MAGONJWA

Posted on: October 3rd, 2022

Na.Catherine Sungura, WAF - KAGERA.

Waganga Wakuu wa Wilaya pamoja na Waratibu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Mlipuko wametakiwa kujidhatiti katika kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola kwa kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa (IDSR).

Hayo yamebainishwa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya afya Dkt. Beatrice Mutayoba wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa kwa timu hiyo ya wasimamizi za halmashauri nane (8) za Mkoa wa Kagera.

Amesema, lengo la kuwajengea uwezo wasimamizi hao ni kujiweka tayari katika kukabiliana na tishio hilo na vilevile na wao kwenda kuwajengea uelewa watoa huduma ngazi za vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo yao.

Aidha, amesema wasimamizi hao pia wataenda kutoa mafunzo kwa watoa huduma ngazi ya jamii na kuwapatia mawasiliano (simu janja) ambayo wataweza kutoa taarifa na tetesi kwenye jamii na kufanya ufuatiliaji kwenye maeneo yao.

“Suala ya ushirikishwaji wa jamii ni muhimu hivyo hawa wasimamizi wakipata elimu hii watashuka chini kwani tunao muingiliano wa kijamii katika biashara na kiuchumi hivyo itawasaidia kutoa taarifa na kupata tetesi na kuzitolea taarifa ngazi ya wilaya”

Sambamba na hilo, amesema mafunzo hayo pia yatawafikia viongozi wa kijiji katika maeneo yote na hivyo itawarahisishia kupata taarifa au tetesi zozote zitakazopatikana katika ngazi ya jamii.

“Tunasema kinga ni bora kuliko tiba hivyo njia za kujikinga ni zile zile ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza, kwahiyo wananchi wazingatie yale wanayoelekezwa na wataalamu na kunawataka wananchi kujenga tabia za kunawa mikono mara kwa mara na sabuni na wanapoona mtu mwenye dalili ni vyema kwenda kituo cha kutolea huduma za afya kilicho karibu.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo amewataka wasimamizi hao kufuatilia na kufanya ukaguzi kwa wasafiri na kuwahusisha zaidi jamii katika kutambua tetesi na kutoa taarifa.