WAGANGA WAKUU WA MIKOA NA HALMASHAURI SIMAMIENI HUDUMA ZA MATIBABU YA MENO KABLA YA KUFIKIA KUNG’OA
Posted on: November 22nd, 2023Na. WAF - Tanga
Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri wametakiwa kuhakikisha wanasimamia matibabu bora ya Kinywa na Meno na kupunguza kung’oa meno bali waongeze watu wanaotibiwa meno.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Novemba 22, 2023 wakati akifungua Kongamano la 38 la kisayansi la Kitaifa na mkutano mkuu wa mwaka wa chama cha wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno linalofanyika Jijini Tanga.
“Mbali na Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri lakini pia Hospitali zote za umma zinazotoa matibabu ya Kinywa na Meno zihakikishe zinaboresha miundombinu ya kliniki za Kinywa na Meno pamoja na kununua vifaa vya kisasa.” Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Takwimu za kuziba meno zimeongezeka kutoka asilimia 2 mwaka 2020 mpaka asilimia 36.1 mwaka 2023 ambapo hali hii imetokana na uwekezaji wa Serikali ya awamu Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema, Takwimu za Mwaka 2022/2023 zinaonesha kuwa watu 541,159 waliooza meno yao ambapo watu 174,749 sawa na 32.3% walizibwa meno yao na watu 323,419 sawa na 59.8% waling'olewa meno yao.
“Kuna Mikoa na Wilaya ambazo zimevuka 60%, nataka nione takwimu za kuziba meno zikiendelea kuongezeka na takwimu za kung’oa meno zikipungua, hali hii iende sambamba na utoaji wa elimu ya kinywa na meno kwa ajili ya kuzuia magonjwa yatokanayo na kukosa elimu sahihi ya kujikinga na magonjwa hayo.” Amesema Waziri Ummy.
Pia, Waziri Ummy amesema katika jitihada za Serikali za kuendelea kufanya mapinduzi Katika Sekta ya Afya imeweza kuajiri wataalam wa Kinywa na Meno 186 na kununua vifaa tiba vya kinywa na meno ikiwemo viti vya kutibia 55 vilivyokwenda kwenye Halmashauri 40 katika Mikoa yote nchini.
Hata hivyo, Waziri Ummy amesema Sambamba na uwekezaji huo, Serikali imeongeza ufadhili wa wataalam wa Sekta ya Afya hasa nafasi za kibingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi kwa kutenga shilingi bilioni 8 ambapo kati ya hizo Tsh. Bil 3 zimetengwa kwa ajili ya kusomesha wataalam kwa seti ili kuleta ufanisi wakati wa utoaji huduma za kibingwa bobezi za Afya.