Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGANGA WAFAWIDHI MKASIMAMIE HUDUMA BORA KWA WANANCHI - WAZIRI UMMY

Posted on: February 14th, 2024



Na. WAF - Dodoma

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka waganga wafawidhi kusimamia ubora wa huduma za Afya zinazotolewa katika vituo vya Afya nchini ikiwa ni pamoja na kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja (Customer Care Desk).

Waziri Ummy amesema hayo leo Februari 14, 2024 wakati akifunga mkutano wa siku Mbili wa waganga wafawidhi ngazi ya msingi uliofanyika katika mji wa Serikali Mtumba Mkoani Dodoma.

“Kwanza mkasimamie ubora wa huduma ambao ni pamoja na kuanzisha madawati ya huduma kwa wateja (customer care desk) ambazo tunaweza kuanza katika hospitali za Wilaya kwa ajili ya kutatua changamoto za wateja, pili tuimarishe maadili ya watumishi kwa kutoa elimu za mara kwa mara na kuhakikisha kamati za maadili vituoni zinafanya kazi.” Amesema Waziri Ummy

Amesema, jambo lingine la kuzingatia kwa waganga hao ni kuhakikisha watumishi walio chini yao wanatoa kauli nzuri kwa wateja kwa kutoa mafunzo ya huduma staha ili wateja waweze kufurahiya huduma kwa kuwa ndio lengo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona Watanzania wanapata huduma bora.

Aidha, Waziri Ummy amemuelekeza Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kukaa pamoja na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) kwa lengo la kuangalia matumizi na makusanyo ya fedha za uchangiaji za Chama cha madaktari.

“Tumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan alituelekeza tupunguze fedha za uchangiaji na angalau zimepungua kidgo ambapo kwa mwaka mnalipa Laki Moja na nusu badala ya laki Mbili.” Amesema Waziri Ummy.