Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGANGA WAFAWIDHI, MADAKTARI BINGWA WATAKIWA KUENDELEA KUVIISHI VIAPO VYAO

Posted on: May 16th, 2024



Waganga Wafawidhi na Madaktari Bingwa wametakiwa kuendelea kuviishi viapo vyao kwa kutambua dhamana Kubwa waliyoibeba katika kuisaidia Serikali kufikisha huduma bora za afya kwa jamii na kutoa Huduma bora kwa watanzania.

Ukumbusho huo umetolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu wakati akizungumza na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa na Madaktari Bingwa leo tarehe 14 Mei, 2024 Jijini Dodoma.

Prof. Nagu amesema Serikali inatambua Kazi kubwa wanayoifanya Madaktari hao na kuongeza kuwa kada ya Udaktari ni wito na kazi iliyo karibu zaidi na Mwenyezi Mungu hivyo amewataka Madaktari hao kukumbuka Viapo vyao.

“Tunaposema huduma za Afya tunamaanisha Matibabu, kinga, utengamao na elimu ya afya kwa umma hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha watanzania wanapata huduma za kinga, na elimu juu ya afya zao Kwa wakati. Serikali kwakutambua kazi kubwa mnayoendelea nayo, nawakumbusha kuendelea kuviishi viapo vyenu hasa kwa kutambua pia hii ni kazi kiimani pia sio maslahi pekee” Amesisitiza Prof. Nagu

Prof. Nagu ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 70 hadi 80 watanzania wanapata huduma za afya kwa ngazi ya msingi hii ni kutokana na uwekezaji wa Serikali kwenye sekta ya Afya na kuwataka Waganga Wafawidhi hao kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwenye Hospitali zao.

“Niwashukuru na kuwapongeza kwa Kazi nzuri na kubwa mnayoifanya , Pamoja na changamoto mbalimbali na mazingira magumu mnayokutana nayo lakini bado mmekuwa mkifanya kazi kubwa kwa weledi Serikali na Wizara ya Afya inatambua mchango wenu na tutazidi kuwapa ushirikiano kwa kila namna mtakavyotuhitaji” ameongeza Prof. Nagu.

Katika kuhitimisha Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Nagu amewataka Waganga Wafawidhi hap kuzingatia Mambo matatu, Mawasiliano mazuri na wagonjwa, Utoaji wa huduma bora kwa Mteja na Kufuta miongozo katika uharaka wa utoaji wa huduma kuzingatia utoaji wa dawa na Matibabu.