Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WAGANGA WA TIBA ASILI WAKUMBUSHWA KUTUMIA MWONGOZO WA RUFAA ZA WAGONJWA

Posted on: August 31st, 2023

Na WAF Dar es Salaam


Waganga wa Tiba Asili/Tiba mbadala kutumia mwongozo wa Rufaa ya wagonjwa ili waweze kupata matibabu stahiki kwa wakati na kuendeleza mahusiano mazuri kati ya wanataaluma wa tiba asili na tiba za kimagharibi


Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Prof. Paschal Ruggajo katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya Tiba Asili ya Muafrika yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Da es Salaam.


Prof. Ruggajo amesema waganga wa Tiba asili wanatakiwa kufahamu na kuchangia katika mnyororo wa Rufaa pale ambapo wagonjwa wanapotambulika ili waweze kuwahi Hospitali.


"Takwimu zinaonesha Kwenye mkoa wa simiyu Takribani asilimia 60 za wagonjwa walioibuliwa na kugundulika wana vimelea vya kifua kikuu walipita kwanza katika waganga wa Tiba asili kwahiyo nawasihi waganga wa tiba asili wawape rufaa wagonjwa kwa yale magonjwa ambayo mgonjwa anatakiwa afikishwe hospitali mara moja na pia amewataka kuwa mabalozi wazuri kwa kuwafikisha wagonjwa Hospitali.


Aidha, Prof. Ruggajo amesema kwa Sasa uchunguzi wa matibabu ambao ni haki ya mteja umeongezeka katika vituo vya kutolea huduma kwa kuwa mgonjwa anaweza kutumia dawa za asili au za kisasa endapo atgundulika anaumwa nini.


"Natoa wito kwa wananchi ambao wanahitaji kutumia huduma ya dawa za tiba asili kwamba sasa zinapatikana katika hospitali za Rufaa za mikoa za Temeke, Mt. Meru-Arusha, Mbeya, Sokou Toure-Mwanza, Bombo-Tanga, Dodoma na Morogoro".


Prof. Ruggajo ameongeza kuwa Huduma hii itamwezesha mteja kuonwa na daktari, kupimwa na baadae kushauriana na daktari matibabu gani yatamfaa.


Prof. Ruggajo amesema Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya maendeleo ya tiba asili hapa nchini ambapo kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala imekamilisha ununuzi wa eneo la ekari 126 katika kijiji cha Mzenga B Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani. 


"Uendelezaji wa eneo hilo unaendelea na pindi litakapokamilika litatoa fursa mbalimbali ikiwemo utunzaji wa miti dawa, mafunzo kwa wataalamu, utafiti, kiwanda cha mfano, uhifadhi wa historia ya tiba asili na mambo mengine mengi". Amesema Prof. Ruggajo.


Vilevile Prof. Ruggajo amesema Serikali imetenga fedha kwa ajili ununuzi wa eneo la kujenga hospitali kubwa au kituo cha umahiri cha tiba asili nchini. 


Nae mganga mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume amewataka waganga wa Tiba Asili/mbadala kutunza mazingira kwa kupanda miti dawa katika maeneo yao.


"Pamoja na jitihada zenu za tiba tujitahidi kupanda miti ambayo itatusaidia kwenye tiba lasivyo tutavuna miti kiholela na miti tiba hii kutoweka". Amesema Dkt. Mfaume.