WADAU WATOA MWELEKEO MPYA WA KUBORESHA LISHE KWA MAMA ANAYENYONYESHA
Posted on: August 5th, 2025
Wadau kutoka sekta mbalimbali za Afya wamekutana Jijini Dodoma kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani na kueleza jitihada zinazofanyila ili kuboresha lishe kusaidia kujenga na kuimarika kwa kwa afya ya mama na mtoto anayenyonyesha.
Wadau kwa nyakati tofauti katika mada zao wamebainisha hayo leo Agosti 5, 2025 ikiwa ni muendelezo wa Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani yanayofanyika kitaifa Jijini Dodoma.
Naye Mkurugenzi wa Ushirikiano na Sera Afrika Mashariki Bw. Gwao Omari, amesema teknolojia mpya ya uzalishaji wa unga wa mahindi na ngano inaleta ubora wa virutubisho kwa maziwa ya mama na lishe bora kwa mtoto.
Kuhusu sekta binafsi Bw. Omari amesema, sekta hiyo inashirikiana kwa karibu na wataalam wa lishe kutoka Halmashauri zote na makubaliano yamefikiwa kuhakikisha wataalam hao wanatoa elimu kwa jamii na kusimamia usindikaji wa vyakula, ikiwemo kiteknolojia na ufundi unaowezesha ufuatiliaji wa hali ya lishe na uzalishaji wa chakula.
“Kupitia ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na wataalam wa lishe kutoka Halmashauri, teknolojia ya kisasa sasa inatumika kuboresha ufuatiliaji na usindikaji wa unga wa ngano na mahindi, ili kuhakikisha chakula chenye virutubisho bora kinawafikia kina mama na watoto kwa ajili ya afya bora,” amesema Bw. Omari.
Kwa upande wake, Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya Bi. Elieth Rumanyika amebainisha kuwa ubora wa maziwa ya mama hutegemea kwa kiasi kikubwa lishe anayopata mama pamoja na mazingira anayoshi huku akisisitiza kampeni mbalimbali zinazoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo ndizo msingi wa kuhakikisha mama anapata chakula chenye virutubisho sahihi.