Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

WADAU WA MAENDELEO TUSHIRIKIANE UTEKELEZAJI WA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Posted on: October 31st, 2024

Na WAF, Arusha.

Rai imetolewa kwa wadau wa maendeleo ya Sekta ya Afya kushirikiana pamoja na Serikali katika kufanikisha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote pamoja na ugharamiaji wa huduma za afya ili huduma bora za afya zipatikane kwa watu wote.

Hayo yamebainishwa Oktoba 30, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Kongamano la Bima ya Afya kwa wote na Jukwaa la ugharamiaji wa huduma za afya lililofanyika Jijini Arusha.

“Ni dhahiri kuwa zinahitajika jitahada za pamoja katika utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa wote. Nitoe rai kwa wadau wote yaani jamii, wadau wa maendeleo, watoa huduma za afya, mashirika ya kijamii na mashirika ya kiraia kuendelea kushirikiana na Serikali katika hatua zote za utekelezaji,” amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema kuwa kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya tiba na huduma za matibabu gharama za matibabu zimeendelea kuongezeka na hivyo kuwafanya wananchi wengi kushidwa kuzimudu huku pia sekta ya afya imeendelea kukabiliwa na upungufu katika mfumo wa ugharamiaji huduma za afya.

“Hatuna budi kushughulikia changamoto hizo na kuhakikisha lengo la huduma bora za afya kwa wote linafikiwa ifikapo 2030. Ili kukabiliana na changamoto hizo, jitihada za pamoja zinahitajika kutoka kwa wadau wote, ndani ya Serikali na wadau wote wa maendeleo. Kongamano hili ni ishara ya ushirikishwaji wa wadau wote muhimu katika kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma katika azma ya kuwa na Taifa lenye afya bora,” amesema Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali imeshaanza kuchukua hatua muhimu za kujidhatiti ili kuimarisha mfumo wa ugharamiaji wa huduma za afya ikiwemo kutungwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ya Mwaka 2023.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya imeendelea kuchukua hatua kuelekea kwenye utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.