WAANDISHI WA HABARI WAJENGEWA UWEZO JUU YA UNYONYESHAJI WA MAZIWA YA MAMA KWA MTOTO
Posted on: August 5th, 2024
Na WAF - Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto, lengo likiwa kuboresha afya ya watoto na akina mama.
Hayo yamesemwa Leo, Agosti 5, 2024 na Bi. Grace Moshi, Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama. Mafunzo haya yamefanyika jijini Dodoma na yanafuata kauli mbiu isemayo "Tatua Changamoto; Saidia Unyonyeshaji wa Watoto kwa Wote."
Bi. Grace ameeleza umuhimu wa lishe bora kwa mama mjamzito na anayenyonyesha, akisisitiza kuwa maandalizi mapema ni muhimu ili kuepuka changamoto kama ukosefu wa maziwa ya kutosha. Alizungumzia pia kuhusu faida za maziwa ya mama kwa afya ya mtoto, na umuhimu wa mtoto kunyonya maziwa hayo kwa miezi sita bila kuongezewa vyakula vingine.
Kwa upande wake, Bi. Elieth Deogratias, Afisa Lishe mwingine, ameongeza kuwa maziwa ya mama yanafaa zaidi kwa umeng'enywaji kwa mtoto mchanga kuliko maziwa ya wanyama. Amehimiza umuhimu wa mtoto kunyonya kwa kuhakikisha amekamata sehemu yote nyeusi ya nyonyo la mama, ili kuepuka maumivu kwa mama na gesi tumboni kwa mtoto.
Bw. Japhet Msoba, Afisa Lishe mwingine, amekanusha dhana potofu kwamba maziwa ya mama yanachacha, akisisitiza kuwa hakuna haja ya kuosha matiti mara kwa mara, kwani inaweza kusababisha michubuko kwa mama au mtoto anaponyonya.
Kwa upande wake, Bw. Paul Mabeja kutoka Nipashe ameishukuru Wizara ya Afya kwa ajili ya mafunzo haya, akisema kuwa yatawasaidia sana katika kufikisha ujumbe kwa wananchi kwa usahihi na kwa wakati muafaka. Ameongeza kuwa mafunzo haya yataimarisha uwezo wa vyombo vya habari katika kutoa taarifa sahihi kuhusu masuala ya afya, hivyo kuchangia kuboresha afya ya jamii kwa ujumla.