Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

VITITA VYA BIMA YA AFYA KWA WOTE (UHI) VIZINGATIE MAHITAJI YA JAMII KWA NGAZI ZOTE

Posted on: July 29th, 2024



Na WAF - Arusha


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ametoa rai kwa wataalam wanaoshughulikia maandalizi ya utekelezaji wa Sheria ya bima ya Afya kwa wote kubuni vitita ambavyo vinazingatia mahitaji ya jamii kwa kujumuisha huduma muhimu ambazo mtu anaweza akazipata na kunufaika nazo kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya juu.


Dkt. Jingu Ameyasema hayo Julai 29, 2024 Jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cha wataalam wa maandalizi ya utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote kinachofanyika mkoani hapo ambapo amesisitiza umuhimu wa wataalamu hao kuangalia huduma ambazo ndio zina tija katika ustawi wa jamii na kuzipa kipaumbele katika vitita watakavyobuni kwa kuendana na mfumo wa rufaa.


“Kitita ambacho tutakibuni, kiwe ambacho kila mtu atapata huduma muhimu, kwa mfano je mama mjamzito kitita kitaweza kumsaidia kuzifikia huduma za juu zaidi au hospitali za juu zaidi iwapo atapata changamoto wakati wa kujifungua, na sio kama kitakuwa na huduma zote ila kibebe zile huduma muhimu kulingana ushahidi au tafiti ,tafiti zetu zinaonyesha nini huduma zipi watu wetu huzitumia mara kwa mara ” Amesema Dkt Jingu


Dkt Jingu ameongeza kuwa iko haja ya kitita kijacho cha bima ya afya kwa wote kuzingatia gharama zinazoweza kuendana na hali ya kipato cha watanzania walio wengi ili kiweze kununulika na kupatikana kwa wepesi kwa watu wa kada zote nchini.


“Gharama ambayo mtaifikiria iwe nafuu, vyovyote itakavyokuwa tuhakikishe kiwe na unafuu kwa watu wetu kwa kuzingatia hali halisi ya uchumi wa watu wetu, Pia Viwango vya Uchangiaji vitavyopendekezwa kwa Kitita cha bima ya afya cha Jamii au Kitita cha huduma muhimu vitawezesha Serikali kutambua kiasi cha fedha kinachohitajika kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.” Amesema Dkt. Jingu.


Ikumbukwe Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ilipitishwa na Bunge tarehe 1 Novemba, 2023 na Mheshimiwa Rais ameidhinisha Sheria hiyo tarehe 19 Novemba, 2023 na imechapishwa katika gazeti la Serikali la tarehe 1 Desemba, 2023.