Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

VIONGOZI WATAKIWA KUIBEBA KAMPENI YA MADAKTARI BINGWA WA RAIS DKT. SAMIA KUFIKISHA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: May 6th, 2025

Na WAF - Songea, RUVUMA


Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma  Bi. Mary Makondo ametoa wito kwa viongozi wote ngazi ya wilaya na halmashauri,  wabunge na madiwani kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Madaktari Bingwa wa Rais Dkt. Samia kwa kuhamasisha wananchi kufika katika hospitali ili kupata huduma za Afya za kibingwa na ubingwa bobezi.



Bi Makondo amesema hayo Mei 26, 2025 mkoani Ruvuma wakati wa mapokezi ya Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi ambapo amesema Serikali imekuwa na utaratibu wa kuwa na kambi za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi kwa mikoa mbalimbali kwa kutumia wataalam wake kutoka ndani na nje ya mkoa.


“Ni ukweli usiopingika kuwa huduma hii ni muhimu kwa jamii yetu hasa kwa vituo vinavyotoa huduma katika ngazi ya afya ya msingi, natoa wito kwa viongozi wote ngazi ya wilaya na halmashauri, Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kutoa ushirikiano wa kutosha kwa madaktari bingwa wetu kwa kuhamasisha wananchi kufika katika hospitali zetu ili  kupata huduma stahiki,” amesema Bi. Makondo.


Amesema kambi hiyo itatoa fursa kwa wananchi kupatiwa huduma stahiki kama ilivyobainishwa kuwa kila hospitali ya halmashauri itapokea seti ya madaktari bingwa sita(6) na muuguzi bingwa mmoja. 



“ Hapa  tuna madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na ukunga, magonjwa ya watoto na watoto wachanga, upasuaji na mfumo wa mkojo, usingizi na ganzi, magonjwa ya ndani, kinywa na meno, masikio, pua na koo na daktari Bingwa wa Mifupa,” amesema Bi. Makondo.


Pia ameelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Sekta ha Afya kwa Mkoa wa Ruvuma.


“Hatuna budi kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya na anayoendelea kuifanya, Katika Mkoa wa Ruvuma Serikali inaendelea kuboresha sekta ya Afya ikiwemo ujenzi na ukamilishwaji wa vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo hospitali ya rufaa ya mkoa, hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati pamoja na ujenzi wa majengo ya huduma za dharura (EMD),” amesema Bi. Makondo.


Amesema kufuatia Mafanikio hayo makubwa yanaleta  Imani kwani Madaktari watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa kwa sababu kuna vitendea kazi na mazingira bora ya kufanyia kazi.