VIONGOZI WA HOSPITALI NA TIMU ZA AFYA SIMAMIENI UBORA WA HUDUMA ZA AFYA KWA WANANCHI
Posted on: November 18th, 2023
Na: WAF, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amewataka viongozi wa Hospitali zote na Timu za Afya nchini kuhakikisha wanasimamia ubora wa Huduma za afya kwa wananchi kwani Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza fedha nyingi katika sekta ya afya nchini.
Dkt. Mollel ameelekeza hayo leo Jijini Dar Es Salaam katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Magonjwa yasiyoyakuambukiza yaliyofanyika katika viwanja vya Hospitali ya Mnazi Mmoja
Aidha Dkt. Mollel amesema ili kuleta tija kwa uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan waganga Wakuu wa mikoa na halmashauri nchini wanatakiwa kuhakikisha wanasimamia vyema ubora wa Huduma za afya katika maeneo yao
“Kwenye Kituo cha kutolea Huduma za afya kilichopo katika halmashauri au mkoa husika hakitoi Huduma bora kwa wananchi mtuhumiwa namba moja utakuwa ni mganga mkuu wa mkoa huo, alafu ndiyo tunaenda kuangalia yule alokosea”. Amesema Dkt. Mollel
Aidha Dkt. Mollel ametoa wito kwa watanzania wote kuhakikisha wanawekeza nguvu kubwa katika kutunza mazingira ili kuepuka milipuko ya magonjwa mbalimbali kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini.
“mvua zinazonyesha kama mazingira sio rafiki maji yatatuama na kusababisha mbu kuzaliana na kuleta malaria lakini pia kama usafi wa mazingira sio mzuri unaweza sababisha kipindupindu”. Amesema Dkt. Mollel
Hata hivyo Dkt. Mollel ametoa rai ya wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara, kufuata utaratibu na ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya kwa kuzingatia ulaji bora ili kuepukana na magonjwa yasiyo yakuambukiza