VIFO VYA UZAZI VYAPUNGUA KANDA YA KASKAZINI
Posted on: December 16th, 2024
Na WAF, Arusha
Vifo vinavyotokana na uzazi na watoto wachanga vimeendelea kupungua kutoka vifo 135 kwa mwaka 2022 hadi vifo 101 mwaka 2023 kwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
Hayo yamebainishwa Desemba 16, 2024 mkoani Arusha na Mkuu wa Idara ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) Dkt. Bariki Mchome, wakati akifungua kikao kazi cha kupokea taarifa na kufanya tathmini pamoja na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kutekeleza afua mbalimbali za kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi, mama na mtoto.
Dkt. Mchome amesema kupungua kwa vifo hivyo kunatokana na jitihada kubwa zinazofanywa na watumishi ambao wanafanya kazi usiku na mchana kuwahudumia wananchi.
“Sote tunafahamu kuwa Serikali imeweka kipaumbele juu ya suala la afya ya uzazi na watoto wachanga na katika kutimiza azma hiyo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Idara ya mama na mtoto ameanzisha huduma za kambi ya matibabu ya madaktari wa mama Samia ambao wanazunguka nchi nzima kuwajengea uwezo kwa vitendo watoa huduma kwenye eneo la huduma za dharura za mama na mtoto na mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro Tanga na Arusha imenufaika,” amesema Dkt. Mchome.
Dkt. Mchome amewataka viongozi wote wa hospitali zilizopo mikoa ya kanda hiyo kupitia kikao hicho kujadili kwa kina sababu zilizochangia vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto
wachanga katika mikoa na halmashauri zao sambamba na kuandaa mikakati madhubuti inayotekezeka.
Awali akitoa salamu za Wizara ya Afya Afisa Program ya Uzazi Salama Dkt. Ulimbakisye Macdonald amesisitiza watumishi wote wa sekta ya Afya kuzidisha uwajibikaji kazini na kwa upande wa viongozi wa hospitali zote nchini kusimamia vyema watumishi hao kwani ni jukumu lao la msingi.
Akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa kikao hicho, mjumbe kutoka mkoa wa Tanga, ambaye ni Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bw. Peter Martin Chambo ameahidi kujikita zaidi kwa kuwa na mikakati bora ya kutekelezaji wa afua zitakazosaidia kupunguza vifo hivyo, wakati wa majadiliano kupitia kikao hicho.